Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akiwa na wamiliki wa viwanda na Watendaji wakuu wa OSHA, WCF NSSF katika ziara ya kufuatilia Sheria za Kazi, Sheria ya Hifadhi ya jamii, Sheria zinazohusiana na Mahusiano kazini pamoja na masuala ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi kwa viwanda vya mkoa wa Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako Wafanyakazi katika kiwanda cha Kansai Plasco Tanzania Ltd na Kiwanda cha Insignia wakati wa ziara ya kufuatilia Sheria za Kazi, Sheria ya Hifadhi ya jamii, Sheria zinazohusiana na Mahusiano kazini pamoja na masuala ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi kwa viwanda vya mkoa wa Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akipa maelezo ya utekeezaji wa Sheria za Kazi, Sheria ya Hifadhi ya jamii, Sheria zinazohusiana na Mahusiano kazini pamoja na masuala ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi kwa viwanda vya mkoa wa Dar es Salaam.
PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU
Na: Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amefanya ziara mkoani Dar es Salaam kwenye Viwandani na kuwataka wamiliki wa Viwanda kuzingatia matakwa ya Sheria za Kazi, Sheria ya Hifadhi ya jamii, Sheria zinazohusiana na Mahusiano kazini pamoja na masuala ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi.
Akiongea baada ya kufanya ziara katika viwanda vitatu vinavyojishuhulisha na utengenezaji wa rangi na mabomba, Mhe. Prof. Ndalichako amebainisha kuwa wamiliki hao wanajitahidi kutekeleza matakwa ya sheria na maelekezo ya serikali lakini yapo mapungufu hawanabudi kuyaboresha zaidi.
“Tumefanya kaguzi na kuona baadhi ya Wafanyakazi hawana vifaa kinga na wengine wanapewa lakini hawavitumii hivyo inabidi wasimamiwe, pia kuna viwanda tumesikia kiwango cha kelele za viwandani zipo juu sana hivyo, kwa mfanyakazi anayeshinda kiwandani inaweza kumuathiri bila kuwa na vifaa husika” alieleza.
Aidha, amefafanua kuwa kwa upande wa Masuala ya Mifuko ya Hifadhi ya jamii Waziri Ndalichako amefafanua kuwa ofisi yake inapata malalamiko ya wastaafu ambapo changamoto zao zinatokana na waajiri wao wa zamani kutotimiza wajibu wao wa kuwalipia michango kwenye mifuko ya Hifadhi ya jamii.
“Serikali tumeamua kufuatilia kwa karibu juu ya michango ya wafanyakazi tunahitaji wazee wapate mafao yao bila usumbufu, tayari kwenye baadhi ya viwanda nimegundua hakuna uwiano kati ya Wafanyakazi wanaolipiwa michango kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF)”
Mhe. Prof. Ndalichako amebainisha kuwa ni muhimu wamiliki wa Viwanda kulipa michango kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa kuwa lengo la Mfuko huo ni kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanaoumia kazini au kupata magonjwa yatokanayo na kazi wanapata mafao bora ya fidia kwa ajili ya kuwawezesha kumudu maisha yao.
Aidha, amebainisha kuwa katika baadhi ya viwanda amegundua wanawatumia Mawakala kuwalipa mishahara wafanyakazi wao, suala ambalo kwa Mawakala wanakuwa wanalitekeleza kinyume cha sheria na usajili wao, ambapo jukumu lao ni kumuunganisha Mfanyakazi na Taasisi. Utartibu huo, huwapa changamoto waajiri kufuatilia juu ya makato ya mshahara kama yanayokatwa kwa mujibu wa sheria.
Amesisitiza kuwa ili kuhakikisha wamiliki wa viwanda wanatekeleza maagizo yake manne yanayo jikita katika kuzingatia matakwa ya Sheria ameekeza Wakala wa Usalama na Afya mahali pa Kazi kunza na viwanda vilivyotembelewa ili watoe ushauri wa kitaalamu kwa ajili ya kuboresha mapungufu waliyobainisha.
“Wataalamu wa WCF na NSSF nao tumewaelekeza waje katika viwanda hivi wafanye ukaguzi wa kina ili kuona kwa nini kunakuwa na utofauti wa michango inayopelekwa NSSF na WCF katka kiwanda kimoja chenye wafanyakazi hao hao wanaopaswa kulipiwa michango yao kwenye mifuko hiyo”
Amewahakikishia kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wamiliki wa viwanda ili waweze kuendelea kufanya biashara nchini, hivyo amewataka wamiliki hao waendelee kuteleza sheria ya mahusiano kazini kwa kuwaruhusu wafanyakazi wao kujiunga na vyama vya Wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi.
Katika hatua nyine; Watendaji wakuu wa Viwanda hivyo, wameishukuru serikali ya Awamu wa Sita kwa jitihada zake za kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kufanya biashara nchini.
Katika ziara hiyo, Mhe. Prof. Ndalichako ameambatana na Kamishina wa Kazi – Suzan Mkangwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtendaji Mkuu Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John K. Mduma pamoja na Mameneja wa NSSF kutoka Dar es salaam na Watendaji waandamizi wa ofisi yake.