Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza rasmi kufunguliwa kwa dirisha la maombi ya udahili kwa waombaji wa shahada ya kwanza kuanzia leo tarehe 8, Julai 2022 badala ya tarehe 15, Julai iliyokuwa imepangwa awali na kwamba dirisha hilo litakuwa wazi hadi hadi tarehe 5 Ogasti mwaka huu.
Akitangaza kufunguliwa kwa dirisha hilo mbele ya waandishi wa habari leo Julai 8,2022 Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Prof. Charles Kihampa amesema kuwa maombi ya udahili ya kujiunga na shahada ya kwanza yanahusu makundi matatu ya waombaji wenye sifa, ambao ni pamoja na sifa stahiki za kidato cha sita, sifa stahiki za Stashahada (Ordinary Diploma), au zinazolingana, na waombaji wenye sifa stahiki za Cheti cha Awali (Foundation Certificate) ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Aidha Tume hiyo imewahimiza waombaji wote wa udahili kuendelea kupata taarifa sahihi kupitia tovuti ya TCU ya www.tcu.go.tz, na tovuti za vyuo zilizoruhusiwa kudahili wanafunzi wa shahada za kwanza, pamoja na taarifa mbalimbali zinazotolewa na TCU kupitia vyombo vya habari.
“Tume inatoa wito kwa waombaji wa udahili na wananchi kwa ujumla kuhudhuria Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yatakayofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja, Dar es Salaam ambapo watapata fursa ya kuonana ana kwa ana na Vyuo vya Elimu ya Juu. Maonesho hayo yatafanyika kuanzia Julai 18 hadi 23, 2022” amesema Prof. Kihampa.
Aidha Prof. Kihampa ameyataja mambo muhimu ya kuzingatiwa na waombaji kuwa ni pamoja na kusoma mwongozo wa udahili uliotolewa na TCU kwa makini na kuelewa kabla ya kuanza kutuma maombi, kutuma maombi moja kwa moja vyuoni kupitia mifumo ya kielektroniki iliyowekwa na vyuo husika, kuwasiliana na vyuo moja kwa moja na kupata taarifa za kina kuhusu program za masomo ili kujiridhisha kabla ya kutuma maombi, na waombaji wenye vyeti vilivyotolewa na mabaraza ya mitihani nje ya nchi ni lazima wawasilishe vyeti vya elimu ya Sekondari au Baraza la taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET)kwa vyeti vya Stashahada ili kupata ithibati ya ulinganifu wa sifa zao kabla ya kutuma maombi ya udahili.
Prof. Kihamapa ametoa wito kwa waombaji wote wa shaha ya kwanza, endapo watahitaji kupata ufafanuzi wa jambo lolote linalohusu udahili, wawasiliane moja kwa moja na vyuo husika, na iwapo watahitaji maelezo ya jumla wanaweza kuwasiliana na TCU kwa kutumia Barua pepe es@tcu.go.tz