Home LOCAL TANZANIA NA KITUO CHA KUDHIBITI MAGONJWA NCHINI MAREKANI (CDC) KUENDELEA KUSHIRIKIANA

TANZANIA NA KITUO CHA KUDHIBITI MAGONJWA NCHINI MAREKANI (CDC) KUENDELEA KUSHIRIKIANA

Na. WAF Dar es Salaam 

Waziri wa Afya Mhe. Ummy  Mwalimu amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa kutoka Marekani katika mapambano dhidi ya magonjwa mbalimbali.  

Waziri Unmy amesema hayo mara baada kukutana na Mkurugenzi wa Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa cha Marekani (CDC) Dkt. Rochelle Walensky na kufanya nae mazungumzo.

Waziri Ummy  ameishukuru CDC kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Mwaka 2001 katika kudhibiti magonjwa ya kuambukiza hususani ugonjwa wa UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria. 

“Tumeshirikiana na CDC katika maneo mbalimbali yakiwemo; kuimarisha huduma za ufuatiliaji wa magonjwa, huduma Za maabara, kuwajengea uwezo wataalam kupitia mafunzo ya muda mfupi na mrefu na kuanzisha mfumo wa kidijitali katika kutoa mafunzo na kutafasiri majibu ya uchunguzi unaofanywa katika vituo vya ngazi ya msingi” amesema Waziri Ummy.

Aidha Mhe Ummy alimfahamisha Dkt Walensky kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan, ameweka kipaumbele katika masuala ya usalama wa afya hususani katika kujikinga, kufanya utambuzi na kukabiliana na mlipuko wa magonjwa na majanga. 

Kuhusu UVIKO-19 Mhe Ummy ameipongeza CDC kwa kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na mlipuko wa UVIKO-19 ikiwemo kuchangia katika kuongeza kasi ya uchanjaji wa chanjo ya UVIKO-19.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha kudhibiti magonjwa cha Marekani (CDC) Dkt. Rochelle Walensky Ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kushirikiana kwa muda mwingi na kuahidi wataendelea kushirikiana kwa kujali Afya za watanzania pamoja na kuongeza msaada kwa Tanzania katika kudhibiti magonjwa na kulinda usalama wa watu duniani kote. 

Dkt. Walensky amesema Kituo hicho hutumia ushahidi wa kisayansi katika kukabiliana na magonjwa hivyo ameishauri Serikali kupitia Wizara ya Afya kuongeza jitihada katika kufanya tafiti za kisayansi zinazohusiana na magonjwa na njia zinazotumika kukabiliana nayo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here