Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco Mkoa wa Singida, Rehema Mwaipopo akizungumzia huduma mpya ya maombi ya kuunganishiwa umeme kwa njia ya mtandao iitwayo NIKONEKT ambayo inafanyika kwa kutumia simu ambapo muombaji anaomba akiwa nyumbani bila ya kufika ofisi za shirika hilo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida limeanzisha utaratibu wa kusikiliza mahitaji na kupokea ushauri wa wananchi na kupokea maoni yao kuhusu sekta ya nishati ya umeme katika wilaya zote ili ziweze kufanyiwa kazi kwa kuwafuata katika maeneo yao.
Meneja wa Shirika hilo Mkoa wa Singida, Mhandisi Florence Mwakasege akizungumza leo Julai 26, 2022 na Wananchi wa Kata ya Iguguno wilayani Mkalama wakati akisikiliza mahitaji na ushauri wao kuhusu sekta ya nishati ya umeme alisema utaratibu huo ambao kwa mara ya kwanza umeanza kufanywa katika kata hiyo akiwa na mwezi mmoja na wiki mbili tu tangu afike mkoani hapa akitokea mkoani Ruvuma kuwa utakuwa endelevu.
“Utaratbu huu utafanyika katika kata na wilaya zote mkoani hapa na ninyi wana Iguguno mmekuwa wakwanza kusikilizwa hivyo tumekuja kuwasikiliza ili tutatue changamoto zenu na kupokea ushauri na maoni yenu tuweze kuboresha huduma za shirika letu ziwe nzuri na kila mwananchi aweze kunufaika nazo” alisema Mwakasege.
Alisema lengo kubwa la mkutano huo ni kuwasikiliza na kupokea ushauri wao na kama kutakuwa na maeneo yenye ukakasi waweze kuyachukua na kuyafanyia kazi ili kila mmoja aweze kutumia huduma hiyo kwa usalama ambayo licha ya kuwa nzuri lakini ikitumika vibaya ni inakuwa ni hatari.
Alisema wao kama wasimamizi wasipowaeleza madhara hayo itakuwa vigumu kuyajua ndio maana wameanzisha utaratibu huo wa kukutana nao ili kufahamishana mambo mbalimbali na kupokea maoni waliyonayo.
Mwakasege alitumia nafasi hiyo kuwashukuru viongozi wa kata hiyo kwa kuratibu mkutano huo pamoja na wananchi ambao walijitokeza kwa wingi na kueleza mahitaji yao mbalimbali.
Katika mkutano huo ambao ulifanyika katika viwanja vya ofisi ya mtendaji wa kata hiyo miongoni mwa mambo yaliyojitokeza kutoka kwa wananchi ni kuomba kupelekewa umeme katika maeneo ambayo hayana huduma hiyo , kupunguziwa gharama za kufungiwa umeme kutoka Sh.27,000 hadi zaidi ya Sh.300,000 ambayo wengi wao hawezi kuimudu .
Katika hatua nyingine wananchi hao walilipongeza shirika hilo Mkoa wa Singida kwa kuanzisha utaratibu wa kwenda kusikiliza mahitaji na ushauri wao na kwa kipekee wakimpongeza Meneja Mwakasege kwa kuanzisha utaratibu huo na kueleza shirika hilo jimejipanga kufanya kazi kwa spidi anayoitaka Rais Samia Suluhu Hassan ya kufanya kazi kwa bidii ili kuwatumikia wananchi.
Wananchi hao walimuambia Meneja wa shirika hilo Mkoa wa Singida, Mhandisi Mwakasege kuwa kutokana na mji wao kuwa mkubwa wapo tayari kutoa eneo la kujenga ofisi ya Tanesco ili waachane na kupanga na wanachotakiwa kukifanya ni kuandika barua ya maombi ya kuomba eneo hilo na kuipeleka ofisi ya kijiji.
Aidha katika mkutano huo Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco Mkoa wa Singida, Rehema Mwaipopo alielezea huduma mpya ya maombi ya kuunganishiwa umeme kwa njia ya mtandao iitwayo NIKONEKT ambayo inafanyika kwa kutumia simu ambapo muombaji anaomba akiwa nyumbani bila ya kufika ofisi za shirika hilo.