Wakii wa kujitegemea na Makamu Mwenyekiti wa MISA – TAN James Malenga akitoa mada kwa waaandishi wa habari za Mtandaoni kuhusu Sheria za Mtandaoni na sheria ya Huduma za habari katika semina yasiku moja iliyoandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) iliyofanyika leo Julai 20,2022 Jijini Dar es Salaam.
Mwandishi wa habari mwandamizi naMkurugenzi wa Fullshangwe Blog John Bukuku (wa pili kushoto) na Mhariri wa habari kutoka Dar 24 Stanslaus Lambat (wa kwanza kushoto) wakiteta jambo.
Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM.
Imeelezwa kuwa utungwaji wa Sheria ya Uhalifu wa Mtandaoni, umebeba maneno yenye ukakasi na yaliyo hatari zaidi kwa mwanahabari.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 20, 2022 na Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA – TAN) Wakili wa kujitegemea James Marenga, katika semina ya siku moja ya waandishi wa Habari za mtandanoni iliyofanyika katika Hoteli ya Sapphire Jijini Dar es Salaam.
Marenga amesema kuwa sheria hiyo ina maneno hatari yanayoweza kumuumiza mwandishi kwa kiwango kikubwa ambapo ametoa angalizo kuwa Sheria hizo zitaumiza wengi endapo kusipokuwepo na umakini.
Amesema, kwa ujumla wake sheria hiyo imeweka baadhi ya maneno ambayo yanaweza kutumiwa vibaya na mahakama huku tafsiri ya maneno hayo ikiwa imefichwa.
Ametaja baadhi ya maneno yenye mitego katika sheria hiyo ni pamoja na ‘kwa namna nyingine’ ama ‘kusudio na kinyume cha sheria.’
“Neno kama ‘kwa namna nyingine ama kusudio na kinyume cha sheria,’ ni maneno hatari yanayotumika hasa kuharamisha jambo ambalo sio kosa kisheria. Maneno haya unaweza kuyaona kuwa ya kawaida, lakini ni hatari sana,” amesema Wakili Marenga.
Kwenye semina na wanahabari hao, Wakili Marenga amesema, kwenye sheria hiyo kuna adhabu zilizowekwa kwa makosa ambayo hayapo wazi kinyume na Ibara ya 13 (6)(C) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia amesema, sheria hiyo kupitia Kifungu 7 (i)(g) iliyotungwa mwaka 2015, imevuruga uhuru wa faragha ambapo taarifa binafsi za mtu zinaweza kuchukuliwa na polisi kinyume na Ibara ya 16(i) ya Katiba ya Tanzania.
“Sheria hii katika Kifungu cha 50(2)(b) kinaondoa haki ya mtu kukata rufaa kinyume na Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba, lakini pia Kifungu cha 38(2)(b) cha sheria hii kinaruhusu usikilizwaji wa shauri mahakamani hata bila muhusika kuwepo”
“Hukumu ikitolewa, ndio unatafutwa na kufungwa bila kujua kesi yako ilipelekwa mahakani lini, na kwa kosa gani. Ndio maana tunasehma sheria hii inatakiwa kupitiwa upya,” amesema Wakili Marenga.