Ugumu wa mwanahabari kupata taarifa anazozitaka kutoka katika taasisi za serikali na umma, unasababishwa na kutokuwepo kwa sheria inayowasukuma maofisa kutekeleza utaratibu huo.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam Julai 19,2022 James Marenga ambaye ni makamu Mwenyekiti wa MISA – TAN amesema, hakuna sheria inayoeleza iwapo Ofisa wa serikali asipotoa taarifa, nini kitafuata.
Kauli ya Wakili Marenga ambaye ni wakili wa kujitegemea, imetokana na kauli ya Gerson Msigwa, Msemaji wa Serikali aliyowataka wanahabari kwenda kupata taarifa wanazozitaka kutoka kwa maofisa habari wa taasisi za serikali, na iwapo watakosa basi waende kwa ‘mabosi’ wao.
Msigwa alitoa taarifa hiyo tarehe 19 Julai 2022, wakati akizungumza kwenye Mkutano wa Utekelezaji wa Miradi ya Maji ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Dodoma.
“Wakati mwingine waandishi tumekuwa tukilalamika, sio lazima umpate mkuu wa taasisi hiyo, Afisa habari amewekwa pale kwa ajili ya kukusaidia,” amesema Msigwa.
Hata hivyo, Msigwa amesema, kutokana na kutokuwepo msukumo kwa maofisa habari ama wakuu wa idara kutoa taarifa, wanahabari wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kupata taarifa hata kama wamefuata utaratibu wa kuomba taarifa hizo.
“Tunaweza kuzungumza kila siku wanahabari wapewe ushirikiano, lakini tatizo linabaki kuwa, maofisa ama wakuu wa idara hata wasipotoa taarifa walizoombwa, sheria haielezi wafanywe nini,” amesema Wakili Marenga na kuongeza:
“Hili ndio linalotusukuma kutaka yafanyike mabadiliko ya sheria za habari kwa kuwa, sheria hii ilivyo haimchukulii hatua ofisa aliyeshindwa kutoa taarifa kwa mwanahabari,” amesema Wakili Marenga.