Home BUSINESS SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA ‘VUMBI LA CONGO’

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA ‘VUMBI LA CONGO’

Na: Rayson Mwaisemba WAF – MOROGORO.

Wizara ya Afya kupitia Baraza la Tiba asili na Tiba mbadala kuanza kuwasaka na kuwachukulia hatua za Kisheria Waganga wa tiba asili na tiba mbadala wanaotoa huduma kwa wananchi bila kusajiliwa na Baraza hilo kuanzia mwezi Februari, 2023.

Hayo yamesemwa leo Julai 27, 2022 na Mwenyekiti wa Baraza hilo Prof. Hamisi Malebo wakati akitoa taarifa ya mwenendo wa utendaji wa Baraza hilo mbele ya Wajumbe wa Baraza hilo na Waandishi wa habari katika Mkoa wa Morogoro.

“Kuanzia mwezi Februari 2023, Baraza litaanza rasmi msako wa waganga ambao wanafanya kazi bila kusajiliwa na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria, lengo ni kulinda afyaza Watanzania.” Amesema Prof. Malebo. 

Amesema, Licha ya jitihada mbalimbali ambazo zimefanyika bado waganga wengi wanafanya shughuli zao bila kusajiliwa kwa mujibu wa kifungu cha 14 na 15 cha Sheria na kwa yeyote anayetoa huduma za tiba asili na tiba mbadala bila kusajiliwa ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 45 (1-3) cha Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala namba 23 ya mwaka 2002. 

Aidha, Prof. Malebo amesema, atakayepatikana na kosa hilo atatakiwa kulipa faini ya shilingi laki tano au kifungo cha miaka miwili au vyote kwa pamoja. 

Hata hivyo, Prof. Malebo amesema, Baraza limeifungia dawa inayoitwa ya Hensha alimaarufu Mkongo yenye usajili namba TZ17TM0027 ambayo ilikutwa imechanganywa na dawa ya kisasa ya nguvu za kiume inayoitwa Sildenafil kwa jina maarufu la biashara ni Viagra ama Erecto, na kusema kuwa Baraza litaendelea kufungia wote wanaofanya kazi kinyume na Sheria. 

“Baraza pia lilibaini dawa inayoitwa Hensha alimaarufu Mkongo yenye usajili namba TZ17TM0027 ambayo ilikutwa imechanganya na dawa ya kisasa ya nguvu za kiume inayoitwa Sildenafil kwa jina maarufu la biashara ni Viagra ama Erecto kitendo hiki ni kinyume na sheria na miongozo ya usajili wa dawa za tiba asili na mbadala.”Amesema.

Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, kuanzia leo tarehe 27 Julai, 2022 limefuta usajili wa dawa ya Hensha alimaarufu Mkongo inayomilikiwa na kituo cha Nyasosi Traditional Clinic na ihakikishe dawa hiyo inaondolewa sokoni mara moja kuanzia leo  vinginevyo hatua kali ya kisheria itachukuliwa dhidi ya Bw. Emmanuel Maduhu. Amesisitiza.

Pia, Prof. Malebo ameweka wazi kuwa,  Kwa mganga ambaye anahitaji kutangaza dawa yake ni lazima afuate utaratibu wa kusajili dawa kwa kupima ubora na usalama na baadaye aombe kibali cha matangazo kutoka Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.

Sambamba na hilo Prof. Malebo amesema, Baraza lilifanya uchunguzi na kubaini baadhi ya dawa kuwa na mapungufu madogo hasa kwenye uandishi wa lebo na vifungashio, na dawa mbili zilibainika kuwa na kiashiria cha hali duni ya usafi wa mazingira ya kutengenezea dawa hizo.

Vile vile, Prof. Malebo amesema, Baraza linaendelea kuwakumbusha wananchi kupata huduma kwa waganga na vituo ambavyo vimesajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na kutumia dawa asili ambazo zimepimwa ubora na usalama pamoja na kusajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala. 

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here