Home LOCAL MSALABA MWEKUNDU WAFIKISHA SALAMU ZA RAIS SAMIA ZA MKONO WA POLE KWA...

MSALABA MWEKUNDU WAFIKISHA SALAMU ZA RAIS SAMIA ZA MKONO WA POLE KWA WAHANGA WA UKAME LONGIDO

Na: Mwandishi Wetu,Longido.

CHAMA Cha Msalaba Mwekundu Tanzania, (Tanzania Red Cross Society), kupitia kwa Rais chama hicho, Mh. David Kihenzile (MB),  wamefikisha salamu za mkono wa pole za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan kwa wahanga wa Ukame Wilayani Longido.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kitengo cha Mawasiliano TRCS, mapema jana Julai 13,  imeeleza kuwa, Mh. Kihenzile ameshiriki zoezi la kugawa fedha na chakula lishe kwa Kaya zilizoathirika na Ukame wilayani Longido Mkoa wa Arusha. 

Ambapo, Mh. Kihenzile amewaeleza wahanga kwamba Msalaba Mwekundu inatimiza jukumu la kuisaidia Serikali kutoa huduma za kibinadamu Nchini. 

Aidha, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kuwa karibu na TRCS na kuiwezeha kuwapatia msaada kaya 159 jumla za jamii za kifugaji Longido, ambapo kila Kaya imepata fedha kiasi cha Tsh 210,000 zilizoathiriwa sana na ukame na wengi wao Mifugo yao kufa.  

Pia Mh. kihenzile amempongeza Mbunge wa Longido, Mh. Dkt. Kiruswa ambaye ni Naibu Waziri kwa Nishati pamoja na Viongozi wote wa Longido kwa ushirikiano mkubwa alioutoa. 

Katika hatua nyingine, Mhe Kihenzile anatarajiwa kuendelea na ziara yake Wilayani Monduli ambapo anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi kwenye zoezi kama hilo.

Zoezi hilo lilianza mapema mwezi Machi mwaka huu, ambapo wataalamu wa TRCS kupitia idara ya Maafa kwakushirikiana na Serikali ya awamu ya sita walifanya tathmini ya waathirika wa Ukame na hatimaye kuungana na shirikisho la Red Cross Duniani kusaidia Kaya hizo ambapo kaya zaidi ya 400 zimenufaika kwa mikoa ya Arusha na Manyara.  

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here