NA:FARIDA SAID, MOROGORO.
Baraza la tiba asili na tiba mabadala nchini limepiga marufuku matumizi na kuifutia usajili dawa ya Hensha maarufu kama MKONGO iliyokuwa na namba za usajili TZ17TM0027 inayomilikiwa na kituo cha Nyasosi Traditional Clinic kilichopo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Morogoro Mwenyekiti wa Baraza hilo Profesa Hamis Masanja Malebo ameleza sababu za kufungiwa kwa dawa hiyo ni kutokana na dawa hiyo kuchanganywa na dawa nyingine ya kisasa aina ya Viagra
Alisema baraza lilibaini dawa hiyo ya Hensha alimaarufu Mkongo ilikutwa imechanganywa na dawa ya iitwayo Slidenafil kwa jina maarufu la biashara Viagra ama Erecto kitendo ambacho ni kinyume cha sheria na miongozo ya usajili wa dawa za tiba asili na mbadala.
Aidha kituo hicho kimetakiwa kuhakikisha inaiondoa sokoni mara moja dawa hiyo ya Mkongo vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mmiliki Emmanuael Maduhu.
Alisema baraza lina wajibu wa kuziondoa dawa ambazo usalama na ubora wake haupo katika viwango sahihi kama ilivyobainishwa kwenye kifungu cha 13(1) cha kanuni ya dawa asili ya mwaka 2008.
Mwenyekiti huyo wa Tiba asili na Mbadala alisema kwa mganga ambaye anahitaji kutangaza dawa yake ni lazima afuate utaratibu wa kusajili dawa kwa kupima ubora, usalama na baade kuomba kibali cha matangazo kutoka baraza.
Aidha amewataka wananchi pamoja na kutumia tiba lishe zinazoboresha afya kuzingatia taratibu na kanuni za afya ili kujikinga na maradhi ya aina mbalimbali.