Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la TEA, Bi. Bahati Geuzye (wa pili kulia) akisisitiza jambo wakati wa kikako cha baraza hilo jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni mwakilishi wa Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa TEA, Bi. Mwanahamis Chambega, Katibu wa Baraza la Wafanyakazi la TEA, Bi. Mwanaisha Komba na kulia ni Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Miradi wa TEA, Bi. Mwafatuma Mohamed.
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la TEA Bi. Bahati Geuzye (wa pili kulia) na viongozi wengine wa Baraza hilo wakifuatialia uwasilishwaji wa hoja kutoka kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi (hawapo pichani) wakati wa kikako cha Baraza hilo Jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni mwakilishi wa Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa TEA Bi. Mwanahamis Chambega, Katibu wa Baraza la Wafanyakazi la TEA Bi. Mwanaisha Komba na Kulia ni Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Miradi wa TEA Bi. Mwafatuma Mohamed.
NA ELIAFILE SOLLA-TEA
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la TEA, Bi. Bahati Geuzye ameupongeza uongozi wa Baraza la Wafanyakazi la TEA kwa jinsi wanavyofanya kazi na kusimamia sheria jambo ambalo linawapa wajumbe wa baraza hilo nafasi ya kujadiliana kwa kina kuhusu mipango na utekelezaji wa shughuli za taasisi.
Alizungumza Haya Katika Kikao Cha Siku Moja Cha Baraza Hilo, Ambacho Kilifanyika Leo Jijini Dar Es Salaam Na Kuhudhuriwa Na Wajumbe Mbalimbali Wanaounda Baraza Hilo, Wageni Waalikwa Ambao Siyo Wanachama Na Mwakilishi Kutoka Chama Cha Wafanyakazi Wa Taasisi Za Elimu Ya Juu (THTU) Makao Makuu.
Mwenyekiti huyo wa Baraza na Mkurugenzi Mkuu wa TEA alisema, tangu kuundwa kwa Baraza hilo wamekuwa na vikao sita, ambapo kila mwaka wamekuwa wakiendesha vikao viwili ambavyo vimefanyika katika mikoa ya Morogoro, Arusha, Pwani, Tanga na Dar es Salaam ambako wamekutana leo.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa, katika miaka mitatu ya uhai wa Baraza hilo, limefanikiwa kufanya kazi zake kikamilifu na kwa weledi wa hali ya juu kwa kuhakikisha vikao vyote vya kisheria vinafanyika kwa lengo la kuhakikisha ushirikishwaji wa wafanyakazi katika maamuzi ya msingi ya Taasisi.
Alibainisha kuwa, Baraza hilo limekuwa linatekeleza majukumu yake kwa ufasaha ambapo, kama sehemu ya majukumu yake ya msingi, limekuwa likishirikishwa katika uandaaji wa maoteo ya bajeti ya TEA kila mwaka na limekuwa likipata taarifa za utekelezaji wa bajeti hiyo, kuangalia mafanikio, changamoto na kisha kutoa mapendekezo ya kuboresha.
Aidha, alisema Baraza hilo linakamilisha muda wake wa utumishi hii leo baada viongozi wake kumaliza kipindi cha utumishi wao ambacho ni miaka mitatu na hivyo Baraza jipya litaundwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.