Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mahafali ya 10 ya Chuo cha Sayansi Kolandoto Manispaa ya Shinyanga yamefanyika leo Ijumaa Julai 29,2022 ambapo Jumla ya wanafunzi 255 wametunukiwa Stashahada na Astashahada katika Programu za Uuguzi na Ukunga, Maabara ya Binadamu , Utabibu , Ufamasia na Ufundi ‘ Laboratory Assistant and Computer Application’.
Mgeni rasmi katikaMahafali ya 10 ya Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto kinachomilikiwa na Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT) alikuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Elias Ramadhani Masumbuko kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema.
Akizungumza wakati wa mahafali hayo, Masumbuko amekipongeza Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto kwa kutoa Programu mbalimbali na kuanza mchakato wa kuanzisha Chuo Kikuu cha Kolandoto akisema ni mipango ya mkoa wa Shinyanga kuanzisha vyuo mbalimbali mkoani humo ili kuongeza fursa za kiuchumi.
“Serikali ya mkoa wa Shinyanga inaendelea kuvutia wawekezaji mbalimbali ili wawekeze katika vyuo ili kuubadilisha mkoa wa Shinyanga…Ni fursa kwenu kuchangamkia fursa ya elimu ya juu sisi mkoa tumejipanga kufanikisha haya”,amesema.