Home LOCAL MAFUNDI UJENZI WA VYUMBA VYA MADARASA ILEMELA KUJENGA KWA NUSUBEI KUUNGA MKONO...

MAFUNDI UJENZI WA VYUMBA VYA MADARASA ILEMELA KUJENGA KWA NUSUBEI KUUNGA MKONO KAMPENI

Na:Paul Zahoro, Mwanza RS

Shule ya Msingi Kahama wilayani Ilemela imepokea kijiti cha kampeni ya Mkoa ya Ujenzi wa vyumba vya madarasa ikiwa ni siku ya tatu tangu ilipoanza ambapo wananchi wamechimba Msingi wa vyumba vya Madarasa 9 katika kukabiliana na msongamano kwenye shule hiyo unaosababishwa na upungufu wa vyumba 38.

Akiongoza kampeni hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amesema changamoto yoyote kwenye jamii inatatuliwa kwa urahisi zaidi endapo watashirikiana wananchi wenyewe kuitatua, na ndio maana Mkoa umeona umalize tatizo la msongamano wa vyumba vya Madarasa kwa kuchangia nguvu wenyewe kwanza na madarasa hayo yakifika hatua fulani basi Serikali itaongezea nguvu. 

“Upungufu wa Madarasa 38 kwenye shule moja inatafsiri kuwa watoto wetu hawana pa kusomea ndio maana tumekuja hapa chini ya kampeni ya Mkoa ya kuanzisha ujenzi wa Madarasa na kukomesha kabisa tatizo hili sugu na Mbunge wetu Mahiri wa Jimbo hili ametupa baraka zote kwani anawapenda sana.”

“Tumeanza  kampeni ya zaidi ya Bilioni 200 tukiwa hatuna hata shilingi moja na tutafanikiwa maana hakuna jambo jema linakwama kwa Mwenyezi Mungu, nawashukuru sana mafundi wangu kwa kuamua kujenga madarasa haya kwa nusu bei.” Mkuu wa Mkoa. 

Pamoja na kutoa Mchango wa Matofali 500 kwenye Ujenzi huo, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mwanza Mhe. Kabula Shitobelo amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa kujitoa sio tu kwa kuanzisha kampeni hiyo bali kuitendea haki kwa vitendo kwani amekua akishirikiana na wananchi kuchimba msingi wa Madarasa kwenye kila wilaya kazi inayofanywa kuanzia saa 11 alfajiri.

Mhe Hassan Masala, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela amebainisha kuwa kwa kushirikiana na Idara ya Elimu zipo taarifa za upungufu wa vyumba vya madarasa 1000 na msongamano upo zaidi kwenye Kata kumi zikiongozwa na Kahama na Buswelu na kwamba wataanzia kwenye maeneo hayo kujenga madarasa.

Meya wa Manispaa ya Ilemela, Mhe. Renatus Mulunga amesema Kata ya Kahama ni hodari wa maendeleo ndani ya kata 19 zilizo kwenye Halmashauri hiyo na kutokana na suala hilo Halmashauri yake itachangia zaidi ya Milioni 2 zilizobakia kukamilisha suala la Kiwanja cha ujenzi wa shule mpya kabla ya kuleta nguvu kubwa kwenye Ujenzi wa madarasa yenyewe.

“Tuna upungufu wa vyumba vya Madarasa 38 kwenye shule ya msingi Kahama na idadi hiyo imetufanya tutafute eneo la kujenga shule ingine na ndipo viongozi na wananchi wa Mtaa huu waliamua kununua eneo hili na tutajenga madarasa 15 hapa na kwenye Mtaa wa Isela tutajenga 15 na pale kwenye shule mama tutajenga vyumba 8” Amesema Masala.

“Suala la ujifunzaji linakua changamoto kutokana na msongamano wa wanafunzi hali ambayo kwenye madarasa mengine wanafunzi wanakaa hadi mlangoni hivyo Ujenzi wa vyumba vipya utasaidia sana na tunakushukuru serikali ya Rais Mama Samia na viongozi wote kwa kuamua kutupunguzia adha hiyo.” Mwalimu Johari Maluba kutoka Shule Msingi Kahama.

Bi. Tedi Shibola amesema kwa kipindi kirefu wananchi wa Mtaa wa Kahama wamekua wakitafakari ni wapi watapata eneo la Kujenga shule ingine maana kumekua na msongamano mkubwa wa wanafunzi kwenye shule ya Msingi Kahama hivyo sasa wanaishukuru serikali kwa kusikia kilio chao na kuja kuanzisha shule mpya ndani ya kata hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here