Home BUSINESS KIWANDA CHA MAFUTA YA ALIZETI KISHAPU KINAVYOMALIZA UPUNGUFU WA MAFUTA

KIWANDA CHA MAFUTA YA ALIZETI KISHAPU KINAVYOMALIZA UPUNGUFU WA MAFUTA

Sehemu ya Kiwanda kidogo cha kusindika mafuta ya alizeti cha Kishapu mkoani Shinyanga

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Mkurugenzi wa Kiwanda cha kusindika mafuta ya kula ya alizeti cha Kishapu, Eliudy Humphrey Urassa amewataka vijana kuchangamkia fursa ya kilimo cha alizeti ili kupata malighafi kwa ajili ya kuzalisha mafuta ya alizeti ikiwa ni sehemu kukabiliana na changamoto ya uhaba wa mafuta kwani viwanda vya kusindika mafuta vipo.

Akizungumza na Maafisa Mawasiliano wa Wizara ya Kilimo na Bodi ya Pamba Tanzania waliotembelea kiwanda chake kilichopo Mhunze wilayani Kishapu Julai 14,2022, Urassa amesema vipo viwanda vikubwa na vidogo vinavyosindika mafuta yatokanayo na mazao kama chake mkoani Shinyanga ambavyo ni suluhisho la kukabiliana na adha ya uhaba wa mafuta nchini.

“Katika Kiwanda chetu cha Kishapu Gold Sunflower cooking oil tunatengeneza mafuta ya asili ya alizeti, mafuta haya hayana kemikali, tunatumia njia za asili kusindika mafuta haya ambapo kwa siku kiwanda hiki kidogo kinazalisha tani moja hadi moja na nusu. Tunashukuru wananchi wengi wanatupa ushirikiano wa kununua mafuta yetu ndani na nje ya wilaya ya Kishapu.

Kwa kweli tumesaidia kupunguza changamoto ya mafuta, Tunauza mafuta kwa bei ya jumla na rejareja kwa bei nafuu sana hata mwananchi akija na kifungashio chake tunamuuzia, bei zetu ni rafiki. Tunauza mafuta hadi lita 20 na tumefanya ubunifu tunavyo vipimo hadi vya shilingi 1000 ili kumwezesha kila mwananchi kutumia mafuta haya”,amesema Urassa.

Urassa ameiomba serikali kuleta mbegu bora iwapatie wananchi ili waweze kuzalisha kwa wingi kwa vile wilaya ya Kishapu ina wakulima wengi wa zao la alizeti na kuhamasisha wananchi kulima mazao yanayotoa mafuta ikiwemo alizeti na pamba ili kupata malighafi kwa ajili ya kuzalisha mafuta ili kuondokana kabisa na uhaba wa mafuta.

Ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali kupitia Mawaziri husika kumpatia nafasi ya kwenda kujifunza masuala ya viwanda nje ya nchi ili kujifunza wabadilike, waongeze maarifa na kuboresha zaidi kiwanda chake hicho kidogo alichokianzisha mwezi Juni,2021 ili kutoa ajira zaidi kwa vijana na sasa wanauza mafuta kwa bei nafuu na kusafirisha mashudu nje ya nchi ikiwemo Rwanda.

Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Kishapu, Emmanuel Kitundu amesema katika wilaya ya Kishapu wapo wajasiriamali wadogo akiwemo Urassa ambao wameanzisha viwanda vidogo vya kusindika mafuta na sasa wanaendelea kuhamasisha wananchi kulima mazao yanayotoa mafuta ikiwemo alizeti na pamba ili viwanda vinavyoanzishwa vipate malighafi na kuondoa uhaba wa mafuta na kushusha gharama za maisha.

Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Joseph Modest Mkude amewapongeza wajasiriamali walioanzisha viwanda vidogo vya kusindika mafuta wilayani Kishapu ambavyo vinapunguza tatizo la upatikanaji mafuta.

“Mwitikio wa kilimo cha zao la alizeti wilayani Kishapu ni mkubwa sana, wananchi wamejitokeza kulima na wengine wameanzisha viwanda vidogo vya kukamua mafuta ya alizeti. Mafuta haya yana nembo ya Kishapu. Sisi kilimo ni biashara, tunalima hapa tunachakata mafuta hapa na kupata bidhaa hapa. Tunachohitaji sasa ni kuwa na vifaa bora zaidi vya kukamua mafuta yote ili kupata mafuta mengi zaidi kwani vifaa vilivyopo kuna mafuta yanapotea”,amesema Mkude.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kishapu, Emmanuel Johnson amesema katika msimu huu wananchi wamelima zao la alizeti na pamba kwa wingi na wataendelea kuhamasisha wananchi kulima kila zao kwani kipaumbele chao katika halmashauri hiyo ni kilimo.

“Tunawahamasisha kujihusisha na kilimo kwani kilimo siyo adhabu, hakuna zao ambalo halina soko, vijana walime ili kujiletea maendeleo na sisi tutaendelea kuwajengea uwezo wananchi walime kwa tija ili wavune kama walivyokusudia. Kilimo ni biashara”,amesema Johnson.

Nao wakulima wa zao la alizeti akiwemo Nyorobi Kasema na Jiyenze Seleli wamesema kiwanda hicho kidogo kimesaidia kupunguza adha ya mafuta kwa wananchi licha kununua mafuta lakini wengi wanapeleka alizeti yao kwenda kusindika na kupata mafuta ya kutumia majumbani mwao.
Mkurugenzi wa Kiwanda cha kusindika mafuta ya kupikia ya alizeti cha Kishapu Gold Sunflower cooking oil mkoani Shinyanga Eliudy Humphrey Urassa akielezea namna kiwanda chake kidogo kinavyosaidia kukabiliana na tatizo la upatikanaji mafuta nchini. Picha na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Kishapu, Emmanuel Kitundu akizungumza ndani ya Kiwanda cha kusindika mafuta ya kupikia ya alizeti cha Kishapu Gold Sunflower cooking oil
Muonekano wa sehemu ya Kiwanda cha kusindika mafuta ya kupikia ya alizeti cha Kishapu Gold Sunflower cooking oil
Muonekano wa sehemu ya Kiwanda cha kusindika mafuta ya kupikia ya alizeti cha Kishapu Gold Sunflower cooking oil
Muonekano wa sehemu ya mafuta yanayozalishwa katika Kiwanda cha kusindika mafuta ya kupikia ya alizeti cha Kishapu Gold Sunflower cooking oil
Muonekano wa sehemu ya mafuta yanayozalishwa katika Kiwanda cha kusindika mafuta ya kupikia ya alizeti cha Kishapu Gold Sunflower cooking oil
Muonekano wa sehemu ya mafuta yanayozalishwa katika Kiwanda cha kusindika mafuta ya kupikia ya alizeti cha Kishapu Gold Sunflower cooking oil
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kishapu, Emmanuel Johnson akielezea fursa mbalimbali zinazotokana na kilimo na kuwataka vijana kuchangamkia fursa katika Kilimo.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Joseph Modest Mkude akielezea faida ya viwanda vidogo wilayani Kishapu na kupongeza wananchi walioanzisha viwanda vya kusindika mafuta ya alizeti.
Mkulima wa alizeti Jiyenze Seleli akielezea namna viwanda vidogo vinavyosaidia kupunguza adha ya mafuta.
Mkulima wa alizeti Nyorobi Kasema akielezea namna viwanda vidogo vinavyosaidia kupunguza adha ya mafuta.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here