MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Abdulrhman Kinana akisalimiana na baadhi ya viongozi MKOANI Katavi alipowsili kwenye ukumbi wa mkutano.
AKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Abdulrhman Kinana ametaja sababu tatu za kwanini Chama hicho kimekaa madarakani kwa muda mrefu na moja ya sababu ni uwepo wa demokrasia ya uhuru watu kujieleza na kutoa maoni yao.
Kinana ametoa sababu hizo leo Julai 25,2022 alipokuwa akizungumza na wana CCM Mkoa wa Katavi wakati wa kikao cha ndani wa wanachama hao wakingozwa na viongozi wa Chama na Serikali ngazi ya Mkoa.
Akizungumza kwenye kikao hicho Kinana amesema kuna watu wamekuwa wakijiuliza kwanini Chama hicho kimedumu muda mrefu.”Sababu ya kwanza lakini kuna demokrasia ndani ya CCM, watu wana uhuru wa kueleza na kutoa mawazo bila hofu bila woga.
“Vikao vya Chama watu wote ni sawa, hata Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa kwenye kikao yeye na wajumbe ni sawa.Hivyo kitu cha kwanza ni demokrasia unatoa nafasi watu kusema, kutoa maoni.Sababu ya pili uhuru wa kuchagua na kuchaguliwa.
“Ndio maana kila kipindi watu wanachagua na kuchaguliwa, kila baada ya miaka mitano nafasi imeisha, nafasi zote zinagombewa hakuna usultani wala ufalme.Hata mimi nawashukuru wajumbe kunichagua kwa kura nyingi. Nafasi yangu ina uzuri na ubaya, anayeteua ni mmoja na anayetengua ni mmoja , asiporidhika huna pauliza, huwezi kushtaki wala kuhoji.Kwa hiyo Chama hiki sifa yake kubwa ni haki ya kuchagua na kuchaguliwa,hakuna mwenye haki miliki.”
Awali akizungumza na wana CCM hao kwenye kikao cha ndani, Kinana amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa kazi kubwa ya kuleta maendeleo ambayo wamekuwa wakiifanya na kwamba mkoa huo umepokea Sh.bilioni 295 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na fedha hizo ameambiwa zimetokana na makusanyo ya mapato mbalimbali ya mkoa.
“Nimepokea taarifa kuhusu namna fedha za maendeleo zinavyotumika vizuri na nataka nieleze hapa Rais Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa na nzuri ya kuleta na maendeleo , Rais wetu sio msemaji sana lakini ni mtu wa vitendo,”amesema Kinana huku akitumia nafasi hiyo kueleza namna akina mama walivyowachapa kazi, wanawake ni mahodari lakini ndio wanalea familia.
Aidha ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wabunge kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya kwani wamekuwa na mchango mkubwa katika kuomba fedha wanapokuwa bungeni kwa kujenga hoja na wamekuwa wakipata fedha hizo ambazo ndizo zinatumika kufanya maendeleo hayo.
“Leo nimetembelea jimbo moja la Nsimbo, Mbunge wa lile jimbo amafanya kazi nzuri sana na nimemwambia ameotesha mizizi kwenda chini itakuwa ngumu kiong’oa lakini naamini na wabunge wengine nao wanafanya kazi nzuri.Pia nawapongeza madwani, watumishi wa umma , wakurugenzi wa halmashauri kwa kazi nzuri mnayofanya.
“Tunathamini kazi zenu, mnafanya kazi katika mazingira magumu na hamna majukwa ya kujitetea. Tunawashukuru mnafanya kazi nzuri sana na sisi tukipata majukwaa tutawasemea,tukiona mahali pameharibika tutasamehe, sio kila mahali unachukua hatua na sisi ni binadamu kuna mahali tunaweza kukosea.
“Madiwani pia tunawashukuru kwa kazi mnayofanya, hawana mshahara lakini wamekuwa wakipata posho ndogo ndogo, CCM tunafanya kazi kwa kujitolea, hata mimi najitolea ukiondoa hii nafasi ya Makamu Mwenyekiti nafasi hii haina mshahara.”