Home BUSINESS ARIPO YATAKIWA KUZIJENGEA UWEZO NCHI WANACHAMA

ARIPO YATAKIWA KUZIJENGEA UWEZO NCHI WANACHAMA

Shirika la Kanda  ya Afrika la Miliki Bunifu (ARIPO) limetakiwa kuendelea kuzijengea uwezo nchi wanachama kuhusu masuala ya Miliki Bunifu ili kukuza uchumi wa kijamii barani Afrika.

Rai hiyo imetolewa leo tarehe 11 Julai, 2022 na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe. Omar Said Shaaban wakati akifungua rasmi mafunzo ya siku tano kwa washiriki 41 kutoka nchi wanachama wa ARIPO yanayofanya katika hoteli ya Verde visiwani Zanzibar. 

Mhe. Shaaban amesema masuala ya Miliki Bunifu hasa hataza ni muhimu katika kukuza ubunifu na uvumbuzi kwani huhamasisha uwekezaji katika utafiti na maendeleo  na hatimaye wahusika kunufaika na vumbuzi hizo.

“Jukumu la kulinda Miliki Bunifu kama hataza, alama za biashara na haki miliki ni nyezo ya kukuza uchumi jamii na maendeleo ya nchi kwa ujumla kwani ulinzi huo unahamasisha uvumbuzi, ubunifu na maendeleo ya teknolojia mpya na wakati huo huo kukuza uwekezaji wa ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji  katika kilimo na viwanda,” amefafanua Mhe. Shaaban.

Mhe. Waziri amesema kuwa imefika wakati sasa masuala ya Miliki Bunifu yafanyike kibiashara ili  nchi za Afrika ziweze kwenda kifua mbele kwenye masuala ya  hataza, alama za biashara na haki miliki. Pia Mheshimiwa Waziri amewaasa ARIPO kwa kushirikiana na Shirika la Miliki Bunifu Duniani kuangalia namna bora ya kusaidia nchi za Afrika ili ziwe na sera bora ya Miliki Ubunifu ikiwa ni pamoja na Tanzania.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Miliki Bunifu  Bw. Seka Kasera ambaye amemwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Godfrey Nyaisa amesema mafunzo haya yanayoyofanyika kwa mara ya pili yana lengo la kuwajengea uwezo wa kuchakata maombi ya hataza na namna ya kutoa ulinzi wa hataza kisheria.

“Tunawashukuru ARIPO kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa nchi wanachama zinajengewa uwezo na kuhimiza kuwa masuala ya hataza yanatakiwa kufanyiwa kazi na  wataalam waliosomea fani ya sayansi ili kuchakata maombi mbalimbali ya hataza kwa ufanisi zaidi,”amefafanua Bw. kasera.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali (BPRA) Bi. Mariam M. Jecha amesema mafunzo haya yana manufaa kwa  taasisi yake na kwa Wazanzibari kwa ujumla hivyo ni matarajio ya BPRA kuwa itayafanyia kazi mafunzo haya na kuhakikisha Miliki Bunifu kwa upande wa Zanzibar zinalindwa kikamilifu.

Mafunzo haya siku tano yanayoshirikisha nchi  zinazozungumza lugha ya  Kiingereza ambazo ni wanachama  wa ARIPO  yamefadhiliwa na Shirika la Kanda ya Afrika la Miliki Ubunifu, Ofisi ya Hataza ya Ulaya na Shirika la Afrika la Haki na Uvumbuzi wa Miliki Ubunifu Africa Intellectual Property Rights and Innovation (AFRIPI) na  European Patent Office (EPO).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here