Home LOCAL WIZARA YA AFYA YAWEKA MKAKATI WA KUCHANJA CHANJO YA UVIKO-19 KWA WANANCHI...

WIZARA YA AFYA YAWEKA MKAKATI WA KUCHANJA CHANJO YA UVIKO-19 KWA WANANCHI 59,000 KWA SIKU

NA: WAF-DAR ES SALAAM.

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani na wadau wa maendeleo na mashirika ya kimataifa imeweka mkakati wa kuongeza kasi ya uchanjaji wa chanjo ya UVIKO-19 nchini kupitia kampeni iitwayo Global VAX Initiatives yenye lengo la kuchanja wananchi 59,000 kwa siku.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Global Vax Initiatives uliofanyika katika viwanja vya Mwembeyanga Temeke jijini Dar Es Salaam.

Waziri Ummy amesema uzoefu uliopatikana katika awamu mbili za utekelezaji wa kampeni umeonyesha kuwa kasi ya matumizi ya chanjo dhidi ya UVIKO-19 huongezeka zaidi wakati wa kampeni na mwenendo wa hali ya uchanjaji hushuka baada ya kampeni na kupelekea Mikoa, Halmashauri na Vituo kutokufikia malengo ya kila siku yaliyowekwa.Tumebaini kuwa baadhi ya walengwa waliopata dozi ya kwanza ya chanjo zinazotolewa kwa dozi mbili hawajarudi kupata dozi ya pili. Mathalani, kwa kipindi cha mwezi Februari, 2022, wananchi ambao hawakurudi kupata dozi ya pili ya chanjo aina ya Sinopharm ni 308,164 (25%), chanjo aina ya Pfizer ni 147,345 (36%) na chanjo aina ya Moderna ni 161,580 (24%)”. Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy ameongeza kutokana na changamoto hizo kuna haja ya kuimarisha mifumo ya utoaji huduma ili matumizi ya chanjo yawe endelevu. Ameongeza kuwa jitihada za kusogeza huduma ya chanjo kwa walengwa wapya zinatakiwa ziende sambamba na kufanya ufuatiliaji kwa waliopata dozi ya kwanza ili kutoa fursa kwa wao kupata dozi ya pili ya chanjo husika.

“Sambamba na kuzindua kampeni hii pia tunapeana maelekezo ya kuongeza kasi ya utoaji wa chanjo dhidi ya UVIKO-19 nchini na kuhakikisha rasilimali fedha zinazotolewa na Serikali na Wadau zinaleta tija iliyokusudiwa nchini”. Amesisitiza Waziri Ummy.

Waziri Ummy ameagiza Wadau Watekelezaji (Implementing Partners, IPs) wote wanatakiwa kushirikiana na Timu za Uendeshaji wa Huduma za Afya ngazi ya Mikoa na Halmashauri katika kuhakikisha afua za chanjo zinatekelezeka ikiwemo huduma mkoba na tembezi, Kuzifikia taasisi au maeneo ya kazi na kutumia matukio mbalimbali, Kuwafuatilia walengwa wote waliohasi chanjo na kuhakikisha wateja wapya wanapata dozi ya pili ya chanjo pamoja na kuhakikisha taarifa za chanjo zinaingizwa kwenye mfumo wa ChanjoCovid System.

Pamoja na hayo Waziri Ummy amesema taarifa mbalimbali za utekelezaji zinaonyesha kuwa, afua za afya ngazi ya jamii ikiwemo chanjo dhidi ya UVIKO-19 hufanikiwa zaidi kwa kuimarisha ushirikishaji wa Viongozi wa Serikali na jamii katika Mamlaka husika hivyo ameomba kushirikiana katika utekelezaji wake.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na Balozi wa Marekani Dkt. Donald Wright, Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Amos Makalla,  Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegello, viongozi mbalimbali wa Serikali na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.

Previous articleWATU 3 MBARONI TUHUMA ZA KUUA MAMA YAO MZAZI WAKITAKA SHAMBA LA URITHI.
Next articleSOMA MAGAZETI YA LEO IJUMAA JUNI 3-2022
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here