Home LOCAL WAZAZI/WALEZI WAMETAKIWA KUWAKATIA BIMA YA AFYA WATOTO WAO

WAZAZI/WALEZI WAMETAKIWA KUWAKATIA BIMA YA AFYA WATOTO WAO

Na. Catherine Sungura,WAF – Dodoma

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewashauri Wazazi na Walezi kuwakatia Bima ya Afya watoto (Afya Toto Card) kwa ajili ya kuwaondolea gharama za matibabu pindi wanapougua ama kupata matatizo ya kiafya.

Kauli hiyo ameitoa wakati akiongea na wananchi waliokua wakipata matibabu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Alisema wakati wanasubiri Sheria ya Bima ya Afya kwa wote (UHC) ambayo itasaidia wananchi wote bila kujali hali zao za maisha kupata huduma zote za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi Taifa ambapo kutawekwa kiwango nafuu.

“Bima ya afya kwa wote itamuwezesha mwananchi yeyote bila kujali hali yake ya maisha na ukiwa na bima hiyo utapata huduma za matibabu pamoja na vipimo kwenye vituo vya afya hadi ngazi ya Taifa”.

Aliongeza kuwa Wizara ya Afya ipo katika hatua za mwisho za kupitisha sheria ya Bima ya Afya kwa wote na kiwango cha kulipia kwa mwaka kitakua ni nafuu ili kumuwezesha mtanzania kupata huduma zote kama anazopata mtumishi wa umma ikiwepo huduma za kulazwa na vipimo mpaka Hospitali ya Taifa.

“Wakati tunasubiri Sheria ya Bima ya Afya kwa wote hivyo ni muhimu wazazi na walezi kuwakatia bima ya afya watoto wao kwa gharama ya 50,400 kwa mwaka na itamuwezesha kupata huduma mpaka ngazi ya Taifa”.

“Kwa sasa Bima hii sio lazima lakini nitakutana na wamiliki wa shule zote za sekondari nchini katika kikao Chao ili tuweke takwa hili la kukata bima ya Afya kwa wanafunzi wa Sekondari.” Alisema Waziri Ummy

Hata hivyo alisema Serikali imechukua hatua hiyo baada ya kuona watoto wakiugua mashuleni wanarudishwa nyumbani kwa ajili v ya matibabu, hivyo akiwa na kadi yake ya Bima ya Afya itamsaidia kupata matibabu popote awe mwanafunzi wa kutwa au wa bweni.

“Tunaanza hatua kwa hatua kama tulivyoanza kwenye vyuo vikuu kwa mwanafunzi kuwa na bima ya Afya ya NHIF na sasa kwa wanafunzi wa sekondari baada ya kuongea na wamiliki wa shule hizo na hata hii ya bima ya Afya kwa wote tumesema hatutawakamata watu kwamba ni lazima pia tunasubiri sheria ipitishwe.” Amesema Waziri Ummy

Katika hatua nyingine Mhe. Ummy Mwalimu amewataka wauguzi katika Hospitali zote nchini kuweka mkakati mzuri wa kuwahudumia wagonjwa kwa muda usiozidi masaa matatu kwa mgonjwa mmoja.

“Watu wanakaa muda mrefu kusubiri kumuona daktari, nimeshamuelekeza mganga mfawidhi waliwekee mkakati, kuanzia ameingia hospital, kumuona daktari na kufanya vipimo kwa kadri inavyowezekana.” Amesema Waziri Ummy

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here