Mkoa wa Geita umepokea Wawekezaji kutoka umoja wa falme za kiarabu Dubai kwa lengo la kuja kuwekeza katika mkoa huo kwenye sekta mbalimbali za kiuchumi.
Wawekezaji hao kutoka Dubai wamefika ndani ya mkoa wa Geita kwa lengo la kujionea na kutembelea maeneo mbalimbali ya uwekezaji katika sekta za kiuchumi zilizopo ndani ya mkoa wa Geita.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Rosemary Senyamule amesema wawekezaji hao wamefika ndani ya mkoa wa Geita na wameonesha nia ya kuwekeza katika maeneo mbalimbali.
Amesema wawekezaji hao wanalenga kuwekeza katika sekita mbali mbali ikiwemo kujenga soko huru la kimataifa la madini ndani ya mkoa wa Geita pamoja na kuwekeza katika sekta ya uchimbaji wa madini,sekta ya utalii, sekta ya elimu, kujenga viwanda vya madawa, viwanda vya chakula katika mkoa wa Geita.
“Baada ya kikao na majadiliano wameonesha shauku ya kuifanya Geita kuwa Dubai ya afrika kwahiyo kwa dhamira ilele sasa leo tuko hapa tunasainiana mikataba nao mikataba ya awali ya namna tutakavyoendelea kuibadilisha Geita katika sekta mbalimbali. Amesema Resemary Senyamule Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mawakili ya United Advocates kutoka Dubai Walid Jumaa akizungumza kwa niaba ya wawekezaji amesema wamevutiwa na maeneo ya uwekezaji yaliyopo ndani ya mkoa wa Geita.
Walid amesema wamevutiwa na nchi ya Tanzania kutokana na kuwa na Vivutio vingi na maeneo mengi ya uwekezaji hivyo wameamua kuja kuwekeza Geita katika sekta za utalii, uchimbaji wa madini, sekta ya elimu, sekta ya afya pamoja na maeneo mengine ndani ya mkoa wa Geita.
Mkurugenzi wa Uhamasishaji uwekezaji EPZA James Maziku ameipongeza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufungua nchi pamoja na kuleta wawekezaji nchini.
Amesema uwepo wa wawekezaji hao ndani ya Mkoa wa Geita utaongeza ukuaji wa uchumi ndani ya mkoa pamoja na kuzalisha ajira kwa wingi katika mkoa wa Geita.