Na. WAF – Morogoro
Wataalamu wa TEHAMA katika sekta ya afya nchini wametakiwa kujiwekea mikakati madhubuti ili kuimarisha zaidi mifumo ya Serikali katika sekta ya Afya.
Hayo ameyasema na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe, leo Juni 28 wakati akifungua kikao kazi cha wataalamu wa TEHAMA kutoka katika taasisi zote za wizara ya Afya kinachofanyika mkoani Morogoro.
“Malengo ya kikao kazi hiki ni kupeana uelewa zaidi juu ya mifumo inayotumika katika kuhakikisha wagonjwa wanahudumiwa kwa wakati, kuweza kuangalia ripoti mbalimbali kwa urahisi, kuhakikisha mifumo imesajiliwa, kuangalia usalama wa taarifa za Serikali na kuhakikisha tunafanyia kazi taarifa ya mkaguzi mkuu wa Serikali CAG.” Amesema Dkt. Shekalaghe
Aidha, Dkt. Shekalaghe amewataka wataalamu hao pindi wanapomaliza kikao kazi hicho waandae maazimio yatakayoonesha mikakati, malengo na changamoto zote kisha waziwasilishe kwake ili maazimio hayo yafanyiwe kazi.
Vilevile Dkt. Shekalaghe ameainisha mambo muhimu ya kuzingatia ambayo ni pamoja na kuweka mkakati mzuri wa kuwahudumia wagonjwa haraka na kwa muda mchache zaidi, Taarifa zipatikane kwa wakati pindi zinapohitajika, Swala la mapato ijulikane wanaolipa hapo hapo na wanaotumia Bima ya Afya.
“TEHAMA ni jambo muhimu sana na Serikali inawaamini ninyi kama wataalamu wa TEHAMA mkafanye kazi kwa uwaminifu na muibebe hii imani mliyopewa.” Amesema Dkt. Shekalaghe
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA wizara ya Afya Bw. Silvanus Ilomo amemshukuru Naibu Katibu Mkuu huyo kuwafugulia kikao kazi hicho na kupokea maelekezo yote aliyowapa.
“Mategemeo yetu baada ya Kikao kazi hiki ni kuhakikisha wataalamu wanapata uwelewa zaidi juu ya uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA ili kufikia malengo tuliyojiwekea na bahati nzuri yamefikia katika hatua nzuri.” Amesema Bw. Ilomo
Ilomo amesema wamepokea maagizo ambayo ni mazuri na watayatengenezea mkakati kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa mgonjwa na kwenda kuyafanyia kazi katika utekelezaji.
Kikao kazi hicho kimehunduriwa na viongozi kutoka wizara ya Afya, mabaraza ya kitaalamu na taasisi zilizopo chini ya wizara ya Afya pamoja na wataalamu wa TEHAMA.