Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Lyidia Shio (kulia) akisikiliza kero na kuchukua taarifa za Mfanyabiashara wa duka la vifaa vya magari katika Kata ya Ilembula iliyopo Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe wakati wa Kampeni ya Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea wilayani hapo.
Afisa Msimamizi wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi.Mercy Macha (kushoto) akisikiliza kero na kuchukua taarifa za Mfanyabiashara wa duka la vifaa vya magari katika Kata ya Ilembula iliyopo Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe wakati wa Kampeni ya Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea wilayani hapo.
Maafisa Wasimamizi wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Lyidia Shio (kushoto) pamoja na Bw. Barnabas Masika (kulia) wakiongea na Afisa Mtendaji Kata wa Ilembula, Bw. Khalid Kapera Wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe wakati wa Kampeni ya Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea wilayani hapo.
Na: Mwandishi Wetu-Njombe.
Wafanyabiashara katika Kata ya Ilembula iliyopo katika Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe wameiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutafuta namna ya kuwasogezea huduma za kikodi ili waweze kulipa kodi zao kwa wakati.
Hayo yamebainishwa na Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi wa TRA, Bi. Lyidia Shio wakati wa Kampeni ya Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea Wilayani hapo ambapo alisema kuwa, baadhi ya mahitaji kwa walipakodi wa eneo hilo ni elimu ya kodi pamoja na kusogezewa huduma ili kuwapunguzia gharama za kusafiri kufuata ofisi ya TRA na kupata huduma ya makadirio kwa ajili ya kulipa kodi zao.
“Niwahikishie kwamba, baadhi ya changamoto za wafanyabiashara wa eneo hili ikiwemo ya umbali na elimu zitafanyiwa kazi kwa haraka ili waweze kulipa kodi zao stahiki kwa wakati na niwaombe tu warasimishe biashara zao kwa kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ili waweze kutambulika na Mfumo wa kodi wa TRA”, alisema Shio.
Akiongea wakati wa Kampeni hiyo, Mtendaji Kata wa Ilembula, Bw. Khalid Kapera amepongeza nia kubwa ya TRA ya kuwatembelea wafanyabiashara wa eneo hilo na kusisitiza kuwa, Elimu hiyo itawafanya wengi wao wawe Mabalozi wazuri kwa wenzao katika kulipa kodi.
“Mimi kama Mtendaji Kata ya Ilembula nawashukuru na nawapongeza kwasababu wafanyabiashara wengi wa hapa wanauelewa mdogo na tofauti kuhusu masuala ya kodi, hivyo ujio wenu hapa wa kuja kutoa elimu utapelekea wafanyabiashara wengi kuwa walipakodi wazuri, lakini pia baadhi ya wafanyabiashara watakua mabalozi wazuri kwa wenzao kwasababu wanatabia ya kuwasiliana”, Kapera.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Wilayani hapo, Bw. Zawadi Nyanginywa ameishukuru TRA kwa kufika katika Kata hiyo na kujionea hali halisi ya ufanyaji biashara katika eneo hilo ikiwemo changamoto za wafanyabiashara hao.
“Nawashukuru sana kwa nyie TRA kufika katika Kata yetu ya Ilembula na kujionea hali halisi ya ufanyaji wa biashara katika eneo hili kwasababu hapo awali kulikua na changamoto nyingi lakini kwa sasa walau ofisi ya TRA ipo Wilayani japo tunahitaji huduma za kikodi ziweze kusogezwa zaidi huku katika kata yetu ili tupunguze gharama za kusafiri kwenda katika ofisi ya TRA kupatiwa huduma”, alisema Nyanginywa.
Nao baadhi ya Wafanyabiashara Wilayani hapo Bw. Justine Mwinuka na Msafiri Chaula wametoa maoni yao tofauti kuhusu zoezi la kampeni ya Elimu ya Mlango kwa Mlango wilayani hapo ambapo wamesema kuwa, matokeo ya ulipaji kodi wanayaona kwani sasa wanaona barabara zinajengwa katika Kata yao pamoja na huduma za afya kuboreshwa na hayo yote yametokana na ulipaji wa kodi.
“Matokeo ya ulipaji kodi kwa sasa tunayaona kwasababu tunaona barabara zinajengwa, vituo vya afya, shule lakini haya yote yanatokana na kodi zetu, niishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kusimamia vizuri kodi zetu na kutuletea maendeleo haya tunayoyaona sasa”, alisema Bw. Justine Mwinuka.
Kampeni ya Elimu kwa Mlipakodi ni mwendelezo wa mkakati wa TRA wa kuhakikisha kwamba Wafanyabiashara nchini kote wanapewa elimu ya kodi ya kutosha na hatimaye waweze kufurahia kulipa kodi zao stahiki na kwa wakati ili Serikali iweze kupata mapato na kuleta maendeleo.
MWISHO.