Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Bw.Kenani Kihongosi akiongoza vijana kwenye matembezi kutoka katika Uwanja wa Benjamini Mkapa mpaka kwenye viwanja vya Muembe Yanga Temeke Jijini Dar es salaam katika uzinduzi wa Uhamasishaji wa SENSA ya Watu na Makazi ambayo itakuwa endelevu kwa nchi nzima. SENSA ya Watu na Makazi inatarajia kufanyika Agosti 23, 2022.
Baadhi ya jumbe za uhamasishaji wa SENSA zilizobebwa na vijana kwenye kwenye matembezi kutoka katika Uwanja wa Benjamini Mkapa mpaka kwenye viwanja vya Muembe Yanga Temeke Jijini Dar es salaam katika uzinduzi wa Uhamasishaji wa SENSA ya Watu na Makazi ambayo ambayo itakuwa endelevu kwa nchi nzima. SENSA ya Watu na Makazi inatarajia kufanyika Agosti 23, 2022.
KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kenani Kihongosi ameomba maelfu ya vijana wa Umoja huo katika matembezi ya uzinduzi wa uhamasishaji wa Watanzania kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi inayotarajia kufanyika Agosti 23 mwaka huu.
Matembezi hayo ya kuhamasisha sensa yamefanyika Leo Juni 23, 2022 kuanzia Uwanja wa Benjamin Mkapa na kumalizikia Uwanja wa Mwembe Yanga wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza akiwa Viwanja vya Mwembe Yanga Katibu MKuu huyo wa UVCCM Kenani Kihongosi amesema kwamba Agosti 23 mwaka huu Watanzania wote watashiriki kwenye Sensa ya Watu na Makazi, hivyo Jumuiya hiyo inayowajibu wa kuhamasisha wananchi wote kushiriki kwenye sensa ifikapo tarehe hiyo.
Amefafanua sensa ya watu na Makazi ndio msingi wa maendeleo ya Taifa letu lakini Sensa inachochea maendeleo, hivyo Serikali inapokwenda kutambua watu wake ni dhahiri itapeleka maendeleo kulingana na idadi ya watu wake katika eneo husika.
“Tumeona baadhi ya maeneo kumekuwa na changamoto, kwanza watu walipohesabiwa mwaka 2012, wengine hawakuhesabiwa, sasa Serikali inapopeleka fedha kama inalenga hospitali, ujenzi wa shule au kuboresha huduma inapeleka kwa idadi ya namba ambayo imeandikishwa“.
“Kumbe idadi ya watu ni kubwa, hivyo sisi Umoja wa Vijana wa CCM wajibu wetu mkubwa ni kuhakikisha tunaungana na Serikali na kuwaleza Watanzania wote wakiwemo vijana wenzetu kwamba sensa ni kitu muhimu na tunaisadia Serikali katika kusukuma ajenda ya maendeleo“.
Kihongosi amesisitiza kwamba vijana wajitokeze kwa wingi ifkapo Agosti 23 ili washiriki sensa lakini waliopo leo kwenye matembezi hayo ni vema wakawa mabalozi wa kuelimisha wengine kuhusu umuhimu wa sensa hiyo. “Mbali ya kufanya matembezi leo hapa tupo na maofisa wa Sensa kutoka serikalini hivyo watatoa elimu kwa wananchi na tunaamini elimu hii itafika kwa wengine.“
Ameongeza kwamba kampeni hiyo itakuwa endelevu na baad ya kuizindua leo mkoani Dar es Salaam itakwenda katika mikoa yote ya Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Kusini, lengo ni kuwakumbusha Watanzania na wajue sensa ina umuhimu mkubwa katika maendeleo.
“Tutakwenda mpaka Zanzibar na kama ambavyo mnafahamu Taifa letu ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuungana Tanganyika na Zanzibar kwa hiyo tunawajibu kufika huko kwa ajili ya kwenda kuhamasisha vijana na Watanzania kuhusiana na suala zima,” amesema Kihongosi.
Akifafanua zaidi kuhusu utoaji elimi ya sensa amesema kuna Wizara ambayo inahusika na masuala ya kuratibu Sensa na katika siku ya leo wamewaita watalaamu hao ili umuhimu wa sensa na sababu za Watanzania kuhesabiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala amesema kwamba tukio hilo la kuhamasisha vijana na wananchi kushiriki Sensa ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa na kampeni hiyo imehudhuriwa na vijana takribani 3000 kutoka wilaya zote za Dar es Salaam na nje ya mkoa huo.
Amesema kwamba kutokana na umuhimu wa Sensa na kutambua fursa za maendeleo zilizopo na ukizingatia Tanzania inasonga mbele wameona wachukue jukumu la uhamasishaji kupitia vijana wenzetu. “Tunasema vijana ni wengi lakini, bila kupata takwimu sahihi sio sawa. Sensa ya mwisho ilikuwa mwaka 2012 na sasa imeshapita miaka 10“.
“Na Tanzania ilikadiriwa kuwa na watu milioni 44, lakini leo tupo takribani milioni 60 bado tunakadiria hatujapata uhakika. Ndio maana tunahamasisha vijana wote bila kujali itikadi za vyama vya siasa wajitokeza kwenye Sensa,” alisema Kilakala na kuelezea “wakati wa sensa utakapofika ni vema kila Mtanzania akishiriki kwa kuhesabiwa na uzuri wa kampeni hii inakwenda kuwakumbusha Watanzania wajibu kwenye jambo hili muhimu kwa Taifa letu.“