Home INTERNATIONAL USAID YATOA TANI 12,000 KWA WAKIMBIZI

USAID YATOA TANI 12,000 KWA WAKIMBIZI

 

 

 

 

 

Na: Selemani Msuya

 

NCHI ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa (USAID), imetoa msaada wa chakula tani 12,000 zinazogharimu Sh.bilioni 20 kwa ajili ya wakimbizi 204,000 walioko katika kambi mbalimbali mkoani Kigoma.

 

Msaada huo kwa wakimbizi 204,000 umekabidhiwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Balozi Dk. Donald Wright.

 

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo wa chakula Balozi Wright alisema wananchi wa Marekani wanatambua changamoto ambazo wakimbizi wanapitia, hivyo kupitia USAID wameamua kutoa msaada huo wa dola za Marekani milioni 9 sawa na Sh.bilioni 20 za Tanzania kununua chakula hicho tani 12,000.

 

Alisema Marekani itaendelea kushirikiana na WFP kuhakikisha wanasaidia wakimbizi kupata chakula na mahitaji mengine muhimu ili waweze kuishi kama binadamu wengine.

 

“Sisi Marekani kupitia USAID tumekuwa tukishirikiana na Serikali ya Tanzania katika mambo mbalinbali, kwa leo tumetoa chakula hiki tani 12,000 ili kikanufaishe wakimbizi 204,000, tunaahidi kuendelea kusaidia WFP ili kundi hili liishi katika maisha ambayo binadamu wengine wanaishi,” alisema.

 

Alisema jambo ambalo wao kama watoa msaada wanajisikia faraja kuona chakula chote hicho kimenunuliwa kwa wakulima wa Tanzania.

 

Balozi huyo alitoa wito kwa wadau mbalimbali kuhakikisha wanasaidia wakimbizi mahitaji mbalimbali ili waweze kuishi vizuri, huku akiwataka wakimbizi ambao wapo tayari kurejea makwao kufanya hivyo.

 

Mkurugenzi Mkazi na Mwakilishi wa WFP nchini Sarah Gordon alisema msaada huo kutoka USAID ni muhimu kwa sababu unaenda kuchochea sekta ya kilimo nchini.

 

“WFP inakabiliwa na upungufu wa fedha tangu 2020, hali ambayo ilipelekea kupunguzwa mgao hadi asilimia 68 chini ya mahitaji, hivyo hali hii imechangia ulaji wa chakula lishe na afya ya wakimbizi kuhusika,” alisema

 

Gordon alisema pamoja na msaada huo kutoka USAID bado WFP haiwezi kutoa mgao kamili kwa wakimbizi kutokana na uhaba wa fedha unaohusiana na idadi ya majanga ya kibinadamu kote duniani.

 

Mkurugenzi huyo alisema USAID ndio mfadhili mkubwa wa operesheni ya WFP kwa wakimbizi nchini ambao wanatoa karibu theluthi moja ya bajati ya kila mwaka, hivyo fedha hizo dola za Marekani milioni 9 zitaweza kusaidia kwa kiasi fulani.

 

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi Wizara ya Mambo ya Ndani, Sudi Mwakibasi alisema msaada huo utaelekezwa kwa wakimbizi wa Nduta na Nyarugusu mkoani Kigoma.

 

“Tumekuwa tukipata msaada wa chakula kwa wakimbizi kutoka nje ila hii tani 12,000 ambazo zimetolewa leo ni mahindi kutoka kwa wakulima wa hapa nchini,” alisema.

 

Mkuu wa WFP Kasulu Nyonzobe Malimi alisema uwezo wa WFP kutoa chakula kwa wakimbizi kwa sasa ni asilimia 68, hivyo wanaomba wafadhili na wadau wengine kusaidia WFP ili waweze kufikia asilimia 100.

 

Malimi alisema katika kuhakikisha WFP inanufaisha wakulima wazawa wamekuwa wakitoa elimu ya kilimo bora.

Credit: Fullshangwe Blog

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here