Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) wametiliana saini ya Makubalino na wakala wa Mabasi yaendayo haraka ili kutoa Huduma za Mabasi hayo katika kipindi cha Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayotarajiwa kuanza rasmi Juni 28, 2022.
Hafla ya kutiliana saini Makubaliano hayo imefanyika leo Juni 6,2022 katika Ofisi za TANTRADE Jijini Dar es Salaam na kuudhuriwa na Maafisa wa Taasisi hizo mbili pamoja na waandishi wa habari.
Akizunza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) Bi.Latifa Khamisi amesema kuwa lengo la kufikia makubaliano hayo ni kuhakikisha kunakuwepo na huduma ya usafiri wa uhakika ili kuwawezesha wananchi kufika viwanjani hapo watakapokuwa wakitembelea maonesho hayo.
Aidha amesema kuwa ipo mikakati waliojiwekea ikiwa ni mipango ya muda mfupi na muda mrefu ambapo katika mpango wao wa muda mfupi ni pamoja na kuweka huduma za maegesho kwa watumiaji wa mfumo wa DART awamu ya pili, pamoja na watumiaji wa Sabasaba, sambasamba na usanifu na uboreshaji wa eneo la sabasaba.
“Kupitia vikao kazi vilivyofanyika baina ya wataamu wa TANTRADE na DART ilikubalika kuwa tuanze na mpango kazi wa muda mfupi ambao utahusisha kuanzisha huduma maalum ya mabasi kipindi cha maonesho ya kimataifa sabasaba ya mwaka 2022”
Na kuongeza kuwa “Washiriki wa Maonesho kuchukuliwa kutoka kituo cha Gerezani moja kwa moja na kuletwa hapa katika Maonesho ya Sabasaba, tunataka wananchi watambue kuna urahisi wa kufika na kuondoka hapa kupitia mabasi ya DART”. Amesema Bi.Latifa.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo kwa haraka (DART), Dkt.Edwin amesema kuwa upo mfumo maalum wa upatikanaji wa tiketi za mabasi hayo ukaokwenda pamoja na tiketi za kuingia katika viwanja vya maonesho hayo ambapo mpango huo utawasaidia wananchi kuondokana na usumbufu wa kupanga foleni ya tiketi kwenye Maonesho hayo.
“Tunajivunia katika ushirikiano huu na TANTRADE na ninaamini litaenda kuleta matokeo makubwa kwa wadau wetu, hivyo wafanyabiashara wote mnakaribishwa na kutumia huduma hii kujitangaza”. Amesema Dkt.Muhede.