Home BUSINESS “TAARIFA ZA WAMILIKI MANUFAA NI KIGEZO CHA UWAJIBIKAJI WA KAMPUNI”

“TAARIFA ZA WAMILIKI MANUFAA NI KIGEZO CHA UWAJIBIKAJI WA KAMPUNI”


Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imewataka Wakurugenzi na Wamiliki wa Makampuni  kuendelea kuwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa kwa wakati ili kuwa na uwazi na uwajibikaji katika kampuni husika.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Sehemu ya Makampuni wa BRELA  Bi. Leticia Zavu, katika warsha maalum  ya uhamasishaji  wadau kuhusu Kanuni za Wamiliki Manufaa, inayofanyika tarehe 08-09 Juni, 2022, katika ukumbi wa Mkapa Soko Matola, Jijini Mbeya.

Bi. Zavu amesema kuwa ushiriki wa wadau katika warsha hiyo unatoa mwanga  katika kuelekea mapinduzi ya uwekezaji nchini, huku akisisitiza kuwa uwajibikaji unaenda sambamba na uwazi katika utekelezaji wa majukumu, jambo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

“Wadau mnapaswa kutoa elimu  hii kwa jamii inayowazunguka, kwani taarifa hizi zinalenga katika  kumfahamu mmiliki halisi na chanzo cha  fedha za kampuni husika,  kwa usalama wa nchi  na  kupunguza mianya ya ubadhilifu miongoni mwa kampuni, hivyo mkawe chachu katika kufanikisha uwasilishaji wa taarifa hizi ndani ya muda uliopangwa,” amesisitiza Bi. Zavu.

Hata hivyo Bi. Zavu amefafanua kuwa  taarifa hizi ni  za siri na wanaozichakata wanazifanyia kazi kwa umakini  hivyo wadau wasiogope kuwasilisha taarifa hizo.

Aidha ameongeza kuwa Mmiliki Manufaa anayepaswa kuwasilisha taarifa zake BRELA  ni yule anayemiliki kuanzia asilimia 5 na zaidi ya uwekezaji kwenye kampuni au kushiriki kufanya maamuzi kwenye kampuni moja kwa moja na taarifa zao zinatakiwa kuwasilishwa kupitia mfumo wa kupokea taarifa za Wamiliki Manufaa unaopatikana kwenye tovuti ya BRELA.

Kwa upande wake Afisa Biashara kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw.Stanley Godwin,   amefurahishwa na mwitikio mkubwa wa wadau walioshiriki warsha hiyo na kuahidi kuwa  ofisi ya mkoa itaendelea kutoa msaada kwa wadau wanaohitaji huduma za  BRELA wakati wote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here