Home LOCAL MRADI WA SH. 540 MILIONI KUONDOA KERO YA MAJI KWA WANANCHI MANISPAA...

MRADI WA SH. 540 MILIONI KUONDOA KERO YA MAJI KWA WANANCHI MANISPAA YA SINGIDA

Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Mulagiri akiangalia mtambo wa kuchimba Visima vya Maji wa  Kampuni ya N & Ground Water Tanzania LTD ya Dodoma ulivyokuwa ukichimba kisima cha mradi wa  Maji Kata ya  Mwankoko uliopo nje kidogo ya Manispaa ya Singida wakati alipotembelea mradi huo jana unaotekelezwa kwa fedha za UVIKO- 19.

Mkurugenzi Mtendaji wa SUWASA Mkoa wa Singida Sebastian Warioba akielezea utekelezaji wa miradi ya maji ya eneo la Mwankoko na Kata ya Unyambwa. Kulia ni Meneja Biashara wa SUWASA Mkoa wa Singida, Hosea Maghimbi na kushoto ni Afisa Ugavi wa SUWASA , Michael Salema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya N & Ground Water Tanzania LTD ya Dodoma iliyopewa zabuni ya kuchimba kisima kimoja cha mradi huo eneo la Mwankoko, Mhandisi Naftal akielezea uchimbaji wa kisima hicho ambapo pia aliishauri Serikali kuwatumia wakandarasi waliosajiliwa na Wizara na wenye uzoefu wa kazi hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya N & Ground Water Tanzania LTD ya Dodoma iliyopewa zabuni ya kuchimba kisima kimoja cha mradi huo eneo la Mwankoko, Mhandisi Naftal (kushoto) akizungumza na Wanafunzi wa Chuo cha Maji Mkoa wa Singida waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo wakati wa uzinduzi wa kisima hicho.

Baadhi ya  Wanafunzi wa Chuo cha Maji Mkoa wa Singida waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo wakati wa uzinduzi wa kisima hicho wakiwa katika picha ya pamoja na Wataalamu wa uchimbaji wa Visima wa Kampuni ya  N & Ground Water Tanzania LTD ya Dodoma.

 Mtambo wa kuchimba Visima vya maji wa  Kampuni ya N & Ground Water Tanzania LTD ya Dodoma ukichimba kisima cha maji cha mradi wa Mwankoko.

Roli likiwa limebeba mabomba ya maji ya mradi wa maji ya Kata ya Unyambwa.
Diwani wa Kata ya Unyambwa, Shabani Magwe akisalimiana na Mhandisi wa Ufundi wa SUWASA Mkoa wa Singida, Richard Kasase wakati akipokea mabomba ya maji yenye thamani ya Sh.83 Milioni wakati akiyapokea jana. Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa SUWASA Mkoa wa Singida Sebastian Warioba.
Diwani wa Kata ya Unyambwa, Shabani Magwe (katikati) akishukuru Serikali baada ya kupokea mabomba hayo.

 Na Dotto Mwaibale, Singida

WANANCHI wa Manispaa ya Singida wataondokana na kero ya maji kufuatia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA)  kuanza kutekeleza mradi wa maji wenye thamani ya Sh.540 Milioni katika Manispaa hiyo.

Mhandisi wa Ufundi wa SUWASA Mkoa wa Singida, Richard Kasase, aliyasema hayo wakati wa uanzaji wa uchimbaji wa kisima cha maji cha  mradi wa Kata ya Mwankoko ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wlaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mulagiri ambaye alikwenda kujionea uchimbaji wa kisima hicho ambacho kinachimbwa kwa fedha UVIKO-19.

Alisema mradi huo utakapo kamilika utaongeza kiwango cha upatikanaji wa maji katika manispaa hiyo kutoka lita za ujazo milioni 10 hadi kufikia lita milioni 12 kwa siku.

“Mahitaji ya maji kwa manispaa ni lita 14 milioni kwa hiyo pamoja na ongezeko hilo litafanya upatikanaji wa maji kufikia asilimia 85.7  kutoka asilimia 71.4 ya sasa,” alisema Kasase.

Kasase alisema mradi huo  unatekelezwa kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Alisema mbali ya mradi huo upo mwingine utakaoanza katika  mwaka wa fedha wa 2022-/2023 wenye thamani ya Sh.Bilioni 1, mwingine ni wa uboreshaji wa huduma ya maji wa miji 28 wa fedha za mkopo wa masharti nafuu kupitia benki ya India ambao ni mkubwa sana na utaongeza visima nane na kuwa unatakribani  kilometa  385.

Wakati huo huo Mkurugenzi Mtendaji wa SUWASA Mkoa wa Singida Sebastian Warioba akipokea mabomba ya mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji  Kata ya Unyambwa alisema mabomba hayo yatalazwa kwenye eneo lenye urefu wakilometa 3.8.

Aliongeza kuwa mabomba hayo yenye kipenyo cha inchi tatu yana thamani ya Sh.83 Milioni na kuwa ni sehemu ya mradi wa maji wa Unyambwa ambao ukikamilika utamaliza kazi ya kuwapatia maji wananchi na kuwa fedha hizo zimetoka kwenye Mfuko wa Taifa wa Maji ambapo katika mwaka huu wa fedha unaokwisha SUWASAilikuwa imetengewa Sh.200 Milioni na mabomba hayo ni sehemu ya kiasi hicho cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya Manispaa hiyo.

Warioba alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo ambazo zimewawezesha kuendelea kutoa huduma ya kuwafikishia maji wananchi wa Manispaa ya Singida.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya N & Ground Water Tanzania LTD ya Dodoma iliyopewa zabuni ya kuchimba kisima kimoja cha mradi huo eneo la Mwankoko, Mhandisi Naftal Mandi aliishauri serikali akisema kuwa  miradi hiyo inakuwa na upotevu mkubwa wa fedha hivyo eneo ambalo linakwenda kufanyika kwa mradi husika linatakiwa usanifu wa kitaalam kwa kuchimba shimo dogo ambalo gharama yake itakuwa ya chini na baada ya kupata matokeo na kubaini kuwepo kwa maji ndipo kazi hiyo inapaswa kuendelea.

“Kwa namna hiyo itasaidia badala ya kuanza kuchimba tu bila ya kufanya usanifu huo ambapo mara nyingi baada ya kufanyika kwa kazi hiyo bila kufanya usanifu huo wanajikuta wametumia fedha nyingi na maji yanakuwa hayapo hivyo Serikali kuingia hasara” alisema Mandi.

Mandi aliishauri Serikali kuwatumia wakandarasi wenye uzoefu wa kutosha kwani sio kila mkandarasi anauwezo wa kufanya kazi hiyo hivyo aliomba wawatumie wakandarasi waliosajiliwa na wizara na kutambulika na jambo hilo likifanyika litasaidia kuokoa fedha nyingi za Serikali zinazopotea kwa kutumia wakandarasi wasio na uzoefu wa kazi hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mulagiri alisema ili upatikanaji wa maji uongezeke kwa wananchi Serikali imetenga fedha za kuhakikisha kila mkoa unapata mitambo ya kuchimba mabwawa na bado wizara itakuwa na mitambo mingine ya kuchimba visima vya namna hiyo na kuwa zoezi hilo la uchimbaji wa visima litakuwa endelevu.


 

Previous articleBRELA, FCC, SIDO KUIMARISHA USHIRIKIANO
Next articleSERIKALI ITAENDELEA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI: NAIBU WAZIRI KIGAHE
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here