Muhidin Amri, Songea.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerai Wilbert Ibuge,amekabidhi pikipiki 286 kwa maafisa ugani waliopo katika Halmashauri nane za mkoa huo ili kuwarahisishia kazi ya kuwahudumia wakulima katika maeneo yao.
Brigedia Jenerali Ibuge alisema,ugawaji wa pikipiki hizo kwa maafisa hao ni moja ya jitihada za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan,katika kuboresha sekta ya kilimo ili iweze kuleta tija katika mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
Alisema,kutokana na changamoto ya wakulima kutofikiwa kwa wakati,wamekuwa hawapati huduma sahihi na kwa wakati kwa kutembelewa mara chache na maafisa hao,licha ya zaidi ya asilimia 87 ya wakazi wa mkoa huo wanategemea kupata riziki zao kutokana na shughuli za kilimo na kuweza kuchangia pato la Taifa na pato la mkoa.
Mkuu wa mkoa alisema,wakulima bado wanalima kilimo cha mazoea kutokana na kukosa wataalam wa kuwapa elimu ya kilimo cha kisasa,hivyo kupatikana kwa pikipiki hizo kutawasaidia sana maafisa ugani na wataalam wengine wa kilimo kuwatembelea wakulima kwa wakati na kuwapa huduma bora ambazo zitawawezesha kuongeza tija katika shughuli zao za kilimo na kukuza uchumi.
Kwa mujibu wa Ibuge,kupitia sekta ya kilimo ambayo ndiyo tegemeo kwa uchumi,mkoa wa Ruvuma ambao umekuwa kinara kwa kuzalisha mazao ya chakula kwa miaka mitatu mfululizo.
Alisema,licha ya uzalishaji wetu kuwa mkubwa,bado uzalishaji umekuwa na changamoto nyingi kutokana na wakulima kulima maeneo makubwa ingawa tija ya uzalishaji kwa eneo imekuwa ndogo.
Ibuge ametaja sababu hiyo, inatokana na wakulima kuendelea kulima kilimo cha mazoea kwa kutopima afya ya udongo na kutopata elimu ya kutosha ya kilimo cha kibiashara.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa, njia mojawapo ya kuondoka hapa tulipo ni kuwawezesha maafisa ugani vifa ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi kwa kuwa changamoto wanayokabiliana nayo ni ukosefu wa vitendea kazi hasa vyombo vya usafiri ili kuwafikia wakulima katika mashamba yao na kuwapatia huduma bora.
Alisema, kwa kutambua changamoto inayowakabili wataalam wa kilimo na ushirika,Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kutoa pikipiki 7000 na vifaa vya kupimia udongo kwa maafisa ugani wa vijiji na kata na kwa maafisa ushirika, ambapo mkoa wa Ruvuma umepata pikipiki 286 kati ya hizo 281 kwa ajili ya maafisa ugani na 5 kwa maafisa ushirika.
Amewataka maafisa ugani na maafisa ushirika waliokabidhiwa Pikipiki hizo,kuhakikisha wanasimamia na kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kuepuka kuzitumia kama biashara kwa kubeba abiria na kufanya shughuli binafsi.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa mkoa huo Stephen Ndaki alisema,Ruvuma ni mkoa wa kilimo hata hivyo bado eneo linalotumika kwa ajili ya uzalishaji ni dogo ikilinganisha na eneo lote linalofaa kwa shughuli hizo.
Alisema,pikipiki hizo zinakwenda kuondoa changamoto katika shughuli za ugani katika wilaya za mkoa huo kwani zitawawezesha maafisa ugani kuwafikia wakulima walioko katika maeneo ya vijijini.
Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema alisema,matumaini ya Serikali ya wilaya na mkoa wa Ruvuma ni kwamba pikipiki hizo zinakwenda kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na kuleta tija kwa wakulima na Serikali.
Awali Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani(RTO)Mkoa wa Ruvuma Salum Morimori,ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuona umuhimu wa kuwapatia maafisa ugani pikipiki ambazo zitarahisisha utendaji kazi kwa wataalam hao wa kilimo ili kuwafikia wakulima katika maeneo yao.
Aidha alisema,madereva watakaoendesha pikipiki hizo watapaswa kuwa na leseni ya kuendesha chombo cha moto baada ya kupata mafunzo kwenye chuo kinachotambulika na Serikali.
Morimori amewaasa watumiaji maafisa ugani na ushirika katika mkoa huo, kujiepusha na ulevi wakati wanapoendesha vyombo vya moto,kubeba abiria zaidi ya mmoja na kuzifanyia matengenezo mara kwa mara ili zidumu kwa muda mrefu.
MWISHO.