Wizara ya Maliasili na Utalii imepongezwa kwa jitihada mbalimbali inazozichukua katika kukabiliana na Wanyama wakali na waharibifu katika makazi na mashamba ya wananchi wanaopakana na maeneo ya hifadhi.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Ally Makoa wakati wa mafunzo ya mbinu mbalimbali za kukabiliana na Wanyamapori waharibifu hasa Tembo yaliyotolewa na Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania ( TAWIRI) katika Kitongoji cha Doma Tarafa ya Mlali Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.
Mhe. Makoa amesema jitihada hizo ziendelee kwa kuwashirikisha wananchi katika utoaji wa elimu ili kuwe na uelewa wa pamoja kuhusu uhifadhi endelevu na usalama wa wananchi.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana licha ya kuishukuru Kamati hiyo ya Bunge amesema Wizara hiyo kwa sasa imeweka mkakati wa kuendelea kushirikiana na viongozi wa Halmashauri za wilaya zenye changamoto ya migongano ya wanyamapori na wananchi kwenye maeneo ya hifadhi pamoja kuimarisha udhibiti wa wanyamapori hao hususani tembo.
Mhe. Chana ameongeza kuwa licha ya elimu kwa wananchi inayotolewa Wizara yake itaendelea kuwadhibiti wanyamapori hao pia kuajiri askari wapatao 600 katika Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu.
Mafunzo hayo ya mbinu za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kwenye mashamba na Makazi ya watu yamekua yakitolewa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali yenye changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu.