Na: Alex Sonna, Fullshangwe Blog -DODOMA
WIZARA ya Fedha na Mipango imeanza kutatua changamoto za wafanyakazi walizoeleza katika baraza la wafanyakazi mwaka jana kwa kutoa mikopo kwa watumishi wake ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 sh.bilioni 1.8 zimetolewa kwa ajili ya mikopo ya usafiri kwa watumishi na zoezi linaendelea.
Kauli hiyo imebainishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Fedha na Mipango Jenifa Omolo wakati akifunga Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo leo Mei 13,2022 jijini Dodoma ambapo amesema kuwa lengo la baraza hilo ni kuhakikisha wanapata maoni na changamoto kutoka kwa wafanyakazi na kujadiliana namna bora ya kushughulikia nazo.
Amesema kuwa baraza la wafanyakazi ni chombo muhimu ambacho kinaiwezesha wizara kupata mawazo ya wafanyakazi ili kuweza kuyafanyia kazi.
Bi.Omolo amesema kuwa pamoja na kupandisha vyeo watumishi wake pia wizara hiyo imetoa kiasi cha Sh. bilioni 1.8 kwa ajili ya kuwapatia mikopo.
“Baraza lililopita watumishi waliwasilisha hoja mbalimbali ambazo walitaka zifanyiwe kazi ikiwemo, maslahi ya watumishi ikiwemo kupanda kwa mshara,kupanda kwa vyeo, kuboresha mazingira ya kufanyia kazi ambayo kwa asilimia kubwa tumeshayafanyia kazi”amesema Omolo
Aidha amesema kuwa suala la nyongeza la mishahara lipo na kwasasa watumishi waiachie serikali kwani inaendelea kushughulikia.
“Tukiwa humu ndani mambo mengi yamejitokeza na kupata majibu ikiwemo suala la kuboresha maslahi ya watumishi,majengo, na ukarabarati wa ofisi za hazina ndogo, nyongeza ya mishahara ambapo suala hili tumesema watumishi waiachie serikali kwani inaendelea kushughulikia nalo,”amesema
Hata hivyo amewataka watumishi wa wizara hiyo kuendelea kufanya kazi na kuhudumia wananchi kwa ufanisi wakati serikali ikiendelea kuzifanyia kazi changamoto zote wanazao kabiliana nazo.
Kwa upande wake Mhasibu Mkuu wa Serikali Leonard Mkude, amewataka wastaafu wote nchini kuwa makini na wimbi la matapeli ambalo limeibuka kutafuta taarifa zao na kuahidi kuwasaidia kwa kuwatoza fedha.
Mkude amesema Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wameanza kuchukua hatua kwa kutoa matangazo mbalimbali lakini kwa upande wa hazina inawataka wastafu wanapopatwa na shida yoyote inayohusu pesheni zao wawasiliane na hazina moja kwa moja katika ngazi ya mkoa au Makao makuu.
“Huduma zetu zote ni bure kama mstaafu anashida atoe taarifa katika ofisi zetu za hazina badala ya kuwasikiliza matapeli ambao wamekuwa wakidai wawapatie kiasi cha fedha ili waweze kuwasaidia katika kulipwa stahiki zao”amesema Mkude.
CTRDIT: Fullshangwe Blog.