Home BUSINESS WAZIRI DKT. KIJAJI AELEZEA MIKAKATI YA WIZARA YAKE KUENDELEZA MIRADI YA KIMKAKATI

WAZIRI DKT. KIJAJI AELEZEA MIKAKATI YA WIZARA YAKE KUENDELEZA MIRADI YA KIMKAKATI

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) amesema katika kipindi cha mwaka 2021/2022 imefufua majadiliano ya mradi wa Bandari na Kanda Maalum ya Bagamoyo (BSEZ) uliosimama tangu mwaka 2018. 

Dkt. Kijaji ameyasema hayo  Mei 6, 2022 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka 2022/2023. 

Amesema wizara inaratibu uendelezaji wa BSEZ unaolenga kuendana na ushindani wa biashara za usafiri wa majini, pamoja na kuunganisha shughuli nyingine za kiuchumi ikiwemo viwanda na utalii. 

Amesema katika mwaka 2021/2022, wizara imefufua majadiliano na wawekezaji wa Kampuni ya China, Merchants Holdings (International) Co. Ltd (CMHI) na Oman Investment Authority (OIA) ambayo awali ilikuwa inaitwa Mfuko wa Uwekezaji wa Serikali ya Oman (SGRF). 

Amesema majadiliano hayo yanahusu eneo dogo la Mradi wa BSEZ kwa kuendeleza hekta 3,087 kati ya hekta 9,887 ambapo unahusisha ujenzi wa Bandari (Sea Port), Kituo cha Usafirishaji chenye hekta 887 na uendelezaji wa Eneo Maalum la Viwanda lenye hekta 2,200. 

“Msingi wa marejeo ya majadiliano hayo ambayo yalisimama mwaka 2018 ni kuhakikisha kuwa Serikali inatekeleza maeneo ambayo ni wajibu wake kama vile ujenzi wa miundombinu wezeshi (barabara, reli, umeme, maji, gesi na mifumo ya mawasiliano) na lango la kuingilia bandarini kwa maslahi mapana ya Taifa,”amesema Dkt. Kijaji. 

Amesema uwekezaji katika maeneo ya Mradi yatafanywa kwa kuvutia wabia wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) au kufanywa na mwekezaji binafsi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here