Musoma.
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Mkoa wa Mara, Msongela Palela amepewa Miezi Mitatu kuongeza kasi yake katika utekelezaji miradi vinginevyo serikali haitaendelea kumvumilia.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa ametoa kauli hiyo Mei 06 Mwaka huu alipofanya ukaguzi na kutoridhishwa na ujenzi wa majengo ya Makao Makuu ya Halmashauri hiyo na Hospitali ya Wilaya katika Kata ya Suguti.
Bashungwa pia ametoa Wiki Moja kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kumpelekea ripoti ya uchunguzi wa miradi inayoichunguza wilayani humo ili afanye uamuzi sahihi dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, John Kayombo ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rufiji Mkoa wa Pwani.
Aidha Mkurugenzi wa Afya ameagizwa kuunda tume itakayoongezea nguvu uongozi wa Mkoa huo, kuchunguza matumizi ya zaidi ya Sh Bilioni 5 zilizopelekwa kwa ajili ya miradi hiyo miwili inayosuasua.
Pamoja na hayo, uchunguzi huo umetakiwa kufuatilia na Sh Milioni 142 ambazo kwa mujibu wa Palela zililipwa kwa njia ya mifumo kwa Kiwanda cha Saruji cha Dangote, kununua Sementi lakini ilielezwa kuwa haikusomeka kiwandani na kwenye mfumo wa halmashauri ilitotoka, hali aliyoielezea kuwa moja ya vyanzo vya ujenzi wa hospitali hiyo kusuasua.
Wakati ujenzi wa makao makuu ukiwa bado kwenye hatua ya msingi, licha ya kupelekewa fedha tangu Mwaka 2019, hospitali ipo katika hatua tofauti za umaliziaji huku wananchi wakilalamikia wizi wa vifaa bila kuchukuliwa hatua yoyote.