Home BUSINESS UPANDISHAJI BEI KIHOLELA NI KOSA LA JINAI: DKT. KIJAJI

UPANDISHAJI BEI KIHOLELA NI KOSA LA JINAI: DKT. KIJAJI

BUNGENI DODOMA.

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji( Mb.) amesema upandaji bei holela ambao kamwe haukubaliki, ni  kosa la jinai na Serikali itachukua hatua za kisheria ili kudhibiti hali hiyo. 

Dkt Kijaji amayasema hayo Mei 6, 2022 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2022/2023. 

Alisema mwenendo wa kupanda bei kusikoendana na uhalisia wa soko ni kati ya changamoto zinazokabili sekta yetu ya biashara ambapo katika kipindi cha kuanzia mwezi Desemba, 2021, kulikuwa na taarifa za uhaba na upandaji wa bei usioendana na uhalisia wa soko kwenye bidhaa za ujenzi, vyakula, nishati na pembejeo za kilimo. 

Amesema Wizara imeendelea kukusanya taarifa za bidhaa sokoni ikiwa ni pamoja na bei za mazao makuu ya chakula na mafuta ya kula katika masoko mbalimbali hapa nchini ili kuwafahamisha wananchi na wadau wengine kuhusu mwenendo wa bei za bidhaa mbalimbali. 

Amesema Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa bei za bidhaa muhimu ikiwemo bei ya mafuta ya kula katika soko la dunia ambayo imeendelea kupanda kutokana na Janga la UVIKO -19 na athari ya vita ya Urusi na Ukraine. 

Akitaja hatua mbalimbali ambazo Serikali imezichukua kudhibiti ongezeko la bei za bidhaa muhimu, Dkt. Kijaji amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine imeendelea kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kutafuta vyanzo mbadala vya upatikanaji wa bidhaa hizo ili kukidhi mahitaji. 

Pia, amesema Serikali imeendelea kuwaagiza  na wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa muhimu kushusha mara moja bei za bidhaa walizopandisha pasipo kuendana na uhalisia wa bei ya soko na kuwaelekeza kuuza bidhaa kwa kuzingatia gharama halisi za uingizaji, uzalishaji na usambazaji. 

Aidha, Dkt Kijaji amesema Serikali inawaelekeza wazalishaji wa bidhaa muhimu kuzalisha na kusambaza bidhaa husika kulingana na uwezo wa viwanda uliosimikwa ili kukidhi mahitaji ya soko. 

Amesema pia Serikali inawaelekeza wauzaji na wasambazaji wa mbolea zenye bei elekezi wahakikishe wanazingatia bei zilizopangwa na Serikali na wale wote watakaokiuka watachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni za biashara. 

Dkt.  Kijaji pia ameielekeza Tume ya Ushindani (FCC) kufuatilia kwa karibu mwenendo wa biashara wa bidhaa muhimu ambazo katika tathmini iliyofanyika zimeonesha kuathirika zaidi na upandaji wa bei na kuchukua hatua za kisheria kwa watakaobainika kukiuka Sheria ya Ushindani ya Mwaka 2003. 

Alisema pia Serikali imeendelea kushawishi na kuvutia Wawekezaji wa ndani na nje katika uzalishaji wa mazao ambayo tumekuwa tegemezi kwa kiwango kikubwa kutoka nje ya nchi ikiwa ni pamoja na mafuta ya kula, sukari na ngano. Lengo likiwa ni kupata uzalishaji unaotosheleza mahitaji ya soko letu la ndani na hatimaye kuuza nje kwa sababu hiyo tunayo kama Taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here