Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi ametoa wito kwa wananchi kuachana na mila na desturi potofu kuhusu hedhi na kusisitiza juu ya upatikanaji wa huduma na vifaa vya kujihifadhi hasa taulo za kike sehemu zote kwa makundi yote kwa bei nafuu katika jamii.
Prof. Makubi amesema hayo leo Mei 27, 2022 wakati akitoa tamko la maadhimisho ya siku ya hedhi salama Duniani akiwa Mkoa wa Tabora.
Amesema, bado jamii ina uelewa mdogo kuhusu suala la hedhi, na kusisitiza ushirikiano katika mapambano dhidi ya mila na desturi potofu kuhusu suala la hedhi, huku akiweka wazi kuwa, hedhi salama ni afya na ni baraka za uumbaji wa Mwenyezi Mungu.
“Bado jamii yetu ina uelewa mdogo kuhusu suala la hedhi hivyo nitoe wito kwa jamii kuachana na mila na desturi potofu kuhakikisha upatikanaji wa huduma na vifaa vya kujihifadhi hasa taulo za kike sehemu zote kwa makundi yote na hata kuwa na bei elekezi katika bidhaa hii.” Amesema Prof. Makubi.
Sambamba na hilo Prof. Makubi amesema, Wizara kwa kushirikiana na wadau inaendelea kutoa elimu na uhamasishaji kwa jamii na shuleni ili kuongeza ufahamu juu ya masuala ya Hedhi Salama.
Aidha, Prof. Makubi amewashukuru wadau mbalimbali kupitia mtandao/Jukwaa la Wadau wa Hedhi Salama (Menstrual Health and Hygiene Coalition – MHH) kwa mchango mkubwa wanaoutoa kuhakikisha suala la Hedhi Salama linatiliwa mkazo pamoja na kupewa kipaumbele.
Mbali na hayo ameweka wazi kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kutoa elimu ya Hedhi Salama kwa jamii kwa lengo la kuhamasisha, kuvunja ukimya na kuachana na mila na desturi potofu kuhusu hedhi na kuhakikisha Sera ya Afya inaliweka jambo la hedhi salama kuwa moja ya vipaumbele ili kutunza heshima na utu wa mwanamke.
Mwisho.