Home LOCAL TANZANIA YAUNGA MKONO JITIHADA ZA SHIRIKA LA AFYA DUNIANI NA MASHIRIKA YA...

TANZANIA YAUNGA MKONO JITIHADA ZA SHIRIKA LA AFYA DUNIANI NA MASHIRIKA YA KIMATAIFA KATIKA KUPAMBANA NA MAGONJWA

 

Na:WAF-Geneva.

Serikali ya Tanzania inaunga mkono jitihada za Shirika la Afya duniani(WHO) pamoja na mashirika mengine ya Kimataifa katika kupambana na magonjwa.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwenye mkutano wa 75l wa Shirika la Afya Dunia unaoendelea jijini Geneva, Uswisi. 

Waziri Ummy ambaye ameongoza ujumbe wa amewasilisha  kauli ya Tanzania ambapo amelipongeza Shirika hilo kwa kutoa ushirikiano kwa wanachama wake na kuunga mkono kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Health for Peace, Peace for Health” yaani “Dumisha Amani, Linda Afya” 

Waziri Ummy amefafanua kwamba kauli mbiu hiyo ni muhimu katika kutambua kuwa, pasipo na amani, utoaji wa huduma za afya mara nyingi huwa hatarini.

“Tanzania inatambua madhara makubwa ya kiuchumi na kijamii yaliyotokana na UVIKO-19, na pia athari zake kwenye mifumo ya afya na maisha ya watu kwa ujumla.Tumeshuhudia mawimbi kadhaa ya mlipuko wa ugonjwa huo na tunatambua kazi kubwa iliyofanywa na Shirika la Afya Duniani katika kuratibu mapambano dhidi ya mlipuko huu, na kuimarisha juhudi za kuboresha utayari wa kukabiliana na dharura na majanga”.Amesema Waziri Ummy.

Hata hivyo amesema kuwa jitihada za pamoja zinahitajika ili kuimarisha uwezo wa sekta ya afya katika utayari wa kukabiliana na dharura na majanga kwa uratibu madhubuti, huku ukizingatia kuwa na mifumo ya afya iliyo thabiti pamoja na mazingira yenye amani. 

Alieleza kuwa Tanzania imejidhatiti katika kuimarisha usalama wa afya katika mwelekeo wa kuhakikisha inafika lengo la Afya kwa Wote.

Aidha, Waziri Ummy alikumbushia kuwa pamoja na nchi kutoa kipaumbele katika kushughulikia janga la UVIKO-19, ni vema nchi zikaendelea na jitihada za kutatua changamoto ya uhaba mkubwa wa watumishi wa Afya.

“Kuongezeka kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza,kasi ndogo ya kupunguza magonjwa ya kuambukiza kama vile UKIMWI na Kifua Kikuu, masula ya Lishe,  Polio, Huduma za Chanjo, pamoja na afya ya akina mama na watoto, tuna imani kuwa mkutano huu utakuwa na mafanikio kwa wote na tunaunga mkono ripoti iliyotolewa na Mkurugenzi wa WHO”.Aliongeza.

Katika kikao hicho, Waziri Ummy amekutana na kufanya mazungumzo  na Bw Atul Gawande, Msimamizi Msaidizi wa Masuala ya Afya ya Kimataifa kutoka Shirika la Msaada la Marekani (USAID) na kukubaliana kushirikiana katika kuimarisha mifumo ya afya iliyo thabiti na endelevu, kutatua changamoto zinazoikabili Tanzania katika eneo la rasilimali watu katika sekta ya afya.

Vile vile Waziri huyo amekutana  na Ujumbe wa Mfuko wa Dunia wa kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) ulioongozwa na Bw. Linden Morrison, Mkuu wa Kitengo cha High Impact Africa II. 

Katika kikao hicho anetumia nafasi hiyo kulipongeza shirika hilo kwa kuzindua kampeni ya awamu ya saba ya kuchangisha fedha zitakazotumika katika kipindi cha utekelezaji kwa mwaka 2023-2025. 

Pia ameufahamisha ujumbe huo kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi la kuwa mmoja wa vinara wa kuhamasisha nchi kuchangia Mfuko huo wakati wa Kampeni.

Kwa upande mwingine Waziri Ummy alikutana na Bw. Ted Chaiban, Mratibu Mkuu wa Ushirikiano katika usamabazaji wa chanjo za UVIKO-19 Duniani na katika mazungumzo yao walikubaliana kuwa ili Tanzania iweze kufikia lengo la kuchanja asilimia 70 ya idadi ya watu wanaolengwa kuchanjwa, ni vema kuongeza idadi ya kampeni za uhamasishaji katika jamii. 

Ushirikiano huo umekubali kutoa fedha za kufadhili kampeni hizo kuanzia mwezi Julai, 2022.

Mkutano huo wa 75 wa Shirika la Afya duniani umemchagua Dkt.Tedros Ghebreyesus kuwa Mkurugenzi wa Shirika hilo kwa mara ya pili kwa kipindi cha miaka minne ijayo 2022-2026.

Mwisho

Previous articleMADIWANI ILALA WAJIPANGA KWA SENSA YA MAKAZI
Next articleYASEMAVYO MAGAZETI ASUBUHI YA LEO ALHAMISI MEI 26-2022
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here