Home LOCAL TABORA KUANZA KUNUFAIKA NA HUDUMA ZA CT SCAN- PROF. MAKUBI

TABORA KUANZA KUNUFAIKA NA HUDUMA ZA CT SCAN- PROF. MAKUBI


Na: WAF -TABORA. 

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema hospitali ya rufaa ya Kitete kuanza huduma za CT Scan hivi karibuni.

Prof. Makubi ametasema hayo leo Mei 27,2022 alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya Serikali kupitia Wizara ya Afya Mkoani hapa.

Amesema kuwa  wananchi wa mkoa huo wataanza kunufaika na huduma hizo, hivyo kupunguza usumbufu wa kufuata huduma kama hizo katika Mikoa mingine. 

“Tangu kupata kwa uhuru wa Tanzania huduma za CT -Scan hazijawahi kuwepo katika Mkoa wa Tabora hii ni historia, hivyo tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiunga mkono Wizara ya Afya kuboresha huduma kwa wananchi”.

Sambamba na hilo, Prof. Makubi ametoa wito kwa Wataalamu na viongozi wa Mkoa kusimamia vizuri vifaa vinavyoletwa na kuweka mkakati mzuri wa matengenezo na maboresho ili vifaa hivyo viwe salama kwaajili ya kuwahudumia wananchi hususan wana Tabora. 

Aidha, Prof Makubi ameileteza uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora Kitete kuhakikisha kabla ya Juni 30, 2022 miradi yote ya ujenzi katika hospitali hiyo iwe imekamilika ili wananchi wa Tabora na Mikoa ya jirani waanze kunufaika na huduma katika miradi hiyo. 

“Natoa maelekezo kwa uongo wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora kushirikiana na uongozi wa Mkoa kuhakikisha miradi yote inayojengwa katika hospitali hii inamalizika kabla ya Juni 30 mwaka huu, na imalizike kwa ubora unaofaa.” Amesema Prof. Makubi. 

Hata, hivyo Prof. Makubi amesema, Changamoto ya uhaba wa dawa nchini inaelekea kuwa historia baada ya kukubaliana na NHIF kuondoa fomu namba mbili C  iliyokuwa ikibagua upatikanaji wa baadhi ya dawa kwa wananchi wanaoenda kupata huduma. 

“Suala la upungufu wa dawa kuwa historia nchini kuanzia Julai 1, 2022, hii ni kutokana na uamuzi wa Serikali kukaa na Mfuko wa Taifa wa bima ya afya na kukubaliana kuondoa fomu namba mbili C iliyokuwa ikitoa mwanya kuonekana uwepo wa Changamoto ya uhaba wa dawa kwa kuruhusu kwenda kununua dawa nje ya kituo. “ Amesema Prof. Makubi. 

Mbali na hayo, Prof Makubi amesema, Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya Watumishi wa afya ,ikiwemo kuongeza mishahara, ujenzi wa nyumba za Watumishi na posho ili kuongeza morali ya kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwa kuwahudumia wananchi. 

Kwa upande mwingine, amesisitiza suala la ubora wa huduma katika  maeneo yote ya kutolea huduma, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Wizara ya Afya katika kuwahudumia wananchi, na kusisitiza kuwa, ubora wa huduma uendane na muda mfupi wa kuwahudumia wagonjwa pindi wawapo katika kituo kupata huduma. 

Pia, ameutaka uongozi wa Mkoa kuendelea kusimamia huduma za wazee katika vituo vya kutolea huduma za afya, ikiwamo kutenga dawati maalum kwa wazee ili kwenda kupata huduma bila malipo kwa wasiojiweza. 

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here