Home SPORTS SHOTOKAN KARATE WAIBUKA WASHINDI WAKIWA WAALIKWA

SHOTOKAN KARATE WAIBUKA WASHINDI WAKIWA WAALIKWA

Wachezaji wa timu ya taifa ya mchezo wa Shotokan Karate wameibuka na ushindi wa tatu (3) katika mashindano ya Kanda ya tano (Zone 5) yanayoandaliwa na Shirikisho la Afrika la mchezo huo waliyoshiriki kama waalikwa, mashindano yaliyofanyika kuanzia tarehe 16 hadi 22 Mei, 2022 nchini Kenya.

Hayo yameelezwa leo Mei 29, 2022 na Katibu wa Chama cha mchezo huo nchini (TASHOKA) Jerome Mhagama kwa njia ya simu wakati timu ikiwa njiani kurejea nchini.

“Awali ya yote tunamshukuru sana Mungu kwa kutusimamia katika safari yetu na kumaliza salama Mashindano kwa ushindi wa nafasi ya tatu  kwa Team KATA (3 Bronze Medals), nafasi ya kwanza imechukuliwa na Madagasca na  nafasi ya pili ni Kenya,”alisema Mhagama na kuongeza kuwa;

“Vijana walipambana kwa moyo sana na kwa uzalendo mkubwa hadi kushika nafasi hii baada ya kuzishinda nchi za Ethiopia, Uganda, Burundi, Somalia, Sudan, South Sudan,  Seychelles, Comoros, Mauritius, Djibouti, Eritrea na Rwanda,”alieleza 

Aidha, Mhagama alieleza kuwa timu yao ilishiriki kama waalikwa kwa heshima ya umaarufu na mchango wa nchi ya Tanzania kwa Nchi nyingi za Afrika na huku akisema kuwa mashindano hayo yanashirikisha mashirikisho ya michezo  na siyo vyama kama walivyoshiriki wao.

“Tumeitumia fursa hii kujifunza mambo mengi,  pamoja na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na viongozi wa ngazi za juu wa UFAK (Union Of Africa Karate Federations) na kuweka mazingira ya tutakapo pata federation yetu wawe tayari kuipokea Tanzania.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TASHOKA na mwalimu wa mchezo huo Yahaya Mgeni ameshukuru ushirikiano wa Serikali kupitia Wizara, Baraza la  Michezo la Taifa (BMT) Ubalozi wa Tanzania Nchini Kenya na Watanzania kwa dua na ufuataliaji wa karibu wa mashindano hayo.

“Mama ameupiga sasa, maana ya kuupiga sana sisi tumekuja Kenya kwa ufadhili wa Serikali kupitia BMT, tunamwahidi Mama hatutamwangusha,”alisema Mgeni.

Timu iliwakilishwa na wachezaji 6 wa Michezo ya Mtu mmoja mmoja (Individual Game) aina ya kumite wanne na Kata wawili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here