Kamishina msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori(Tawa)Kanda ya Kusini Abraham Jullu kushoto na kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Kamishina msaidizi Joseph Konyo wakiangalia meno ya Tembo yaliyokamatwa katika kijiji cha Hanga wilayani Namtumbo baada ya watu wasiofahamika kuyatelekeza baada ya kustukia mtego wa kuwakamata.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma Kamishina msaidizi Joseph Konyo na Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Uhifadhi wanyamapori(Tawa)kanda ya kusini Abraham Jullu wakionyesha meno ya Tembo kwa Waandishi wa Habari(hawapo pichani) yaliyokamatwa wilayani Tunduru hivi karibuni ambapo jumla ya watu watatu wanashikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na meno hayo.
Afisa wa Jeshi la uhifadhi wanyamapori(Tawa)kanda ya kusini Deogratius Chami,akipanga vipande vya meno ya Tembo yaliyokamtwa katika kijiji cha Milonde wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kabla ya kuonyeshwa kwa waandishi wa Habari,
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Kamishina msaidizi Joseph Konyo akionyesha vitu mbalimbali vilivyokamatwa na Jeshi hilo kufuatia misako na operesheni za kuwakamata watu wanaojihusisha na matukio ya uharifu zinazoendelea kufanyika katika wilaya zote za mkoa huo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Kamishina msaidizi Joseph Konyo akionyesha mafuta ya kula kwa waandishi wa Habari(hawapo pichani) yaliyokamatwa na Jeshi hilo kufuatia misako na operesheni mbalimbali zinazofanywa dhidi ya vitendo vya kiharifu na waharifu katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma.
Na: Muhidin Amri, Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori (Tawa) kanda ya kusini, limewakamata watu watatu wakazi wa wilaya ya Tunduru wakiwa na meno tisa na vipande vinane vya meno ya Tembo.
Kamanda wa Polisi mkoani humo Kamishina msaidizi Joseph Konyo aliwataja watu hao kuwa ni Said Awadi,Hassan Hakimu na Zakaria Rashid na walikamatwa tarehe 10 Mei 2022 majira ya saa mbili usiku katika kijiji cha Milonde-Kiuma.
Kamanda Konyo alisema,meno hayo yana uzito wa kg 20.4 na thamani yake ni Sh. milioni 138,600,000 ambapo watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika.
Aidha Konyo alisema,Jeshi la Polisi na askari wa Tawa wamefanikiwa kukamata meno Matano ya Tembo yenye uzito wa kg 44 yenye thamani ya Sh.103,950,000.
Alisema,meno hayo yalikamatwa katika kijiji cha Hanga- Monastery wilayani Namtumbo, baada ya kutelekezwa na watu ambao walistukia mtego uliowekwa na Polisi na askari wa Jeshi la Uhifadhi,hata hivyo jitihada za kuwatafuta na kuwakamata zinaendelea.
Kwa mujibu wa Kamanda Konyo,jumla ya Tembo saba waliuawa katika matukio hayo mawili na kila tembo mmoja ana thamani ya Dola za Kimarekani 1,500 sawa na pesa za Kitanzania Sh.milioni 242,550,000 kwa Tembo wote.
Alisema,kupatikana kwa nyara hizo na kukamatwa kwa watu hao kunatokana na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Jeshi la Polisi na Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori(Tawa).
Kwa upande wake Kamishina msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori(Tawa)kanda ya kusini Abraham Jullu,amewataka wananchi kuepuka vitendo vya uwindaji haramu wa wanyamapori wakiwamo Tembo ambao ni rasilimali na tunu kubwa za Taifa.
Alisema,uvunaji(uwindaji) haramu wanyamapori ni kosa kisheria kwani wanyama hao wanalindwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kuvutia wageni na Watanzania wanaokwenda kutembelea Hifadhi za Taifa na kutoa fedha ambazo zinazochangia kukuza uchumi wa nchi yetu.
Alisema,Tawa na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vitahakikisha inawakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakojihusisha na vitendo vya uwindaji haramu.
Kamishina Jullu, ameitaka jamii kusaidiana na mamlaka husika kulinda rasilimali zilizopo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,badala ya kutanguliza maslahi binafsi.
Katika hatua nyingine Kamanda Konyo alieleza kuwa,kuanzia tarehe 1 hadi 12 Mwezi huu Jeshi hilo limefanya operesheni maalum iliyolenga kuwakamata watu wanaojihusisha na matukio ya uvunjaji,wizi na wapokeaji wa mali za wizi katika maeneo mbalimbali.
Kamanda Konyo alisema,katika operesheni hiyo wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa kumi na sita kati yao wanaume kumi na tatu na wanawake watatu wakiwa na vitu vya wizi.
Alitaja vitu vilivyokamatwa ni Televisheni kumi,Radio Subwofer nne,spika moja,magodoro mawili,mitungi mitano ya Gesi,viti vya Plastiki kumi,ndoo hamsini za mafuta ya kula,kitanda,mabegi ya nguo na baiskeli moja.
Ametoa onyo kwa watu wanaojihusisha na shughuli za ujangili na matukio ya wizi kuacha mara moja, kwani Jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama havitawafumbia macho.
MWISHO.