Imeelezwa kuwa, wahariri wa vyombo vya habari nchini kwa kupitia vyombo vyao wana nafasi kubwa ya kufanikisha ukuaji wa Sekta ya Biashara nchini kwa kutoa uelewa mpana kwa wananchi kuweza kurasimisha biashara zao.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji katika kikao kazi cha siku mbili kati ya wahariri wa vyombo vya habari na BRELA kilichoanza leo Mei 21, 2022 mkoani Morogoro, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Hashil Abdallah amesema kuwa, anaamini kuwa wahariri wakijengewa uwezo juu ya majukumu ya Brela kutasaidia jamii kupata elimu hiyo.
“Kwa muktadha huu niwaombe wahariri tushirikiane kwa pamoja kwenye kufanikisha ukuaji wa sekta ya biashara nchini, hasa wananchi warasimishe biashara zao. Kupitia nyie watakuwa na uelewa wa mambo mengi,”amesema Dkt.Abdalah kwa niaba ya Waziri Dkt.Kijaji.
Na kuoneza kuwa, “BRELA, muelewe kuwa wahariri wana jukumu la kuandika habari kwa usawa, pindi wanapotaka kutoa habari kwenu msiwe wagumu kutoa taarifa, kama majibu ya maswali yao yapo kwa muda huo wapewe ili umma upate taarifa kwa haraka na kama habari wanayohitaji inachukua muda kupata majibu wapewe mrejesho mapema ili waweze kusubiri ili upotoshaji usiwepo,”aliongeza.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni, (BRELA) Godfrey Nyaisa amesema kuwa, usimamiaji wa majukumu ya msingi ya BRELA umewezesha kuwa na mafanikio makubwa yenye uwazi na ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Aidha Nyaisa amesema kuwa, hali hiyo inatokana na uboreshaji wa mazingira ya biashara na urahisishaji wa sajili na leeni zinazotolewa na BRELA hapa nchini.
“Mafanikio haya yametokana na utekelezaji wa mikakati mikuu ya Kitaifa, Sera na Mpango wa Maendeleo ya Taifa,”amesema Bw,Nyaisa.
PICHA MBALIMBALI ZA WAHARIRI KATIKA KIKAO KAZI HICHO.