Home BUSINESS BRELA WAPATIWA MAFUNZO YA AFYA

BRELA WAPATIWA MAFUNZO YA AFYA

Tume   ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imewata  Watumishi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni(BRELA), kulinda afya zao pamoja na  kuangalia mienendo ya maisha yao ya kila siku ili kuepuka magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na msongo wa mawazo na kufanya afya ya akili kuwa imara.

Rai hiyo imetolewa na Mtaalam wa Afya ya Akili kutoka TACAIDS. Bi. Violeth Ndosi, tarehe 14 Mei, 2022, wakati wa mafunzo kuhusu Virusi vya UKIMWI na UKIMWI, Magonjwa Sugu yasiyoambukiza na Afya ya Akili mahala pa kazi, katika ukumbi wa  jengo la PSSF lililopo Mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam.     

  Bi.  Ndosi  ameeleza kuwa karibia asilimia 50  ya msongo wa mawazo unatokea mahali pa kazi na hii ni kutokana na watumishi kutotimiza wajibu wao na kutokujali muda. 
Ameongeza kuwa ni vizuri kila mmoja akawa balozi wa maisha yake katika kujali afya, kujali watu wanaomzunguka, kujali kazi na nafasi yake kazini kwani yote haya yakitimizwa yatasaidia kupunguza msongo wa mawazo na kufanya afya ya akili kuwa imara.

 Bi. Ndosi ameongeza kuwa maisha ya sasa yamebadilika kutokana na utandawazi  kwani watu wanajali sana shughuli zao na kukosa muda wa kukaa karibu na familia zao.

Amefafanua kuwa kutokana na hali hiyo malezi ya watoto yamekuwa ni changamoto na kusababisha vijana wengi kuathirika kisaikolojia kutokana na mazingira wanayoishi. 


“Sasa hivi kumekuwepo na ongezeko la wavuta bangi, mashoga, wanaojiuza pamoja na vibaka jambo ambalo si jema kwa ustawi wa jamii na ndiyo chanzo kimojawapo cha maambukizi ya virusi vya UKIMWI na UKIMWI,”alifafanua Bi. Ndosi.

Pia Bi. Ndosi amewataka watumishi kutenga muda kwa ajili ya mazoezi pamoja na kuzingatia mlo kamili wa kila siku ili kuwa na afya bora.

Kwa upande wake Dkt. Patrick Kanyamwenge kutoka TACAIDS akiwasilisha mada kuhusu magonjwa sugu yasiyoambukiza   amesema kuwa yapo magonjwa mengi sugu yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiathiri mwenendo wa maisha ya kila siku, hivyo ni vyema watumishi wakitambua afya zao mapema na kuweka mipango madhubuti ya kuhakikisha Afya zao zinaendelea kuwa imara.

Dkt. Kanyamwenge ametoa ufafanuzi wa aina mbalimbali ya magonjwa yasiyoambukiza yanavyoathiri watu wengi na kusababisha hata kuharibu  mfumo wa maisha yao kiujumla. 

Aidha Dkt. Kanyamwenge ameeleza kuwa magonjwa haya yamekuwa yakiathiri sana mfumo wa maisha na kusababisha wengi kutofikia malengo pamoja na ndoto zao ambayo ni pamoja na kisukari, moyo, figo, saratani na mengine mengi.

Dkt. Kanyamwenge Amewataka  watumishi wa BRELA kupima afya zao mara kwa mara na kuzingatia mienendo ya maisha yao ya kila siku, ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukizwa.

Akifunga mafunzo haya ya siku moja, Mkurugenzi wa Huduma na Uwezeshaji Bw. Daimon Kisyombe  amemshukuru Dkt. Kanyamwenge pamoja na Bi. Ndosi  kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa kwa kuthamini afya za watumishi kwa kuwapatia elimu juu ya VVU, UKIMWI,magonjwa sugu  yasiyoambukiza na Afya ya Akili mahala pa kazi.
Previous articleSIMBA YATINGA NUSU FAINALI YA KOMBE LA AZAM
Next articleBRELA YAIBUKA MSHINDI WA PILI KATIKA MAONESHO MOROGORO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here