Home Uncategorized AFISA JESHI LA ULINZI LA WANANCHI WA TANZANIA ( JWTZ) ATUNUKIWA...

AFISA JESHI LA ULINZI LA WANANCHI WA TANZANIA ( JWTZ) ATUNUKIWA NISHANI YA UTENDAJI BORA NA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI ( CISM)

Na: Meja Selemani Semunyu.

Kanali Joseph Bakari, Mkurugenzi wa Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (CISM) ametunukiwa Nishani iitwayo OFFICER kwa kutambua moyo wa, kujituma, bidii na juhudi zake katika kuendelea michezo Jeshini ikiwa ni sehemu ya kutekeleza malengo ya CISM  kutumia shughuli za michezo na utimamu wa mwili  kueneza amani duniani.  

Kwa Mujibu wa Mtandao wa CISM Nishani hiyo ya Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani International Military Sports Council -CISM),yenye Makao yake makuu Jijini Brussels Nchini Ubelgiji, imetolewa wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka ulioanza tarehe 01 Mei, hadi  tarehe 9 Mei 22 Jijini Lima Peru.

Mkutano huo ambao ni wa  kwanza kwa wanachama kukutana uso kwa uso  tangu mwaka 2019 kutokana na janga la Uviko 19, uliohudhuriwa na nchi wanachama 65 kutoka katika mabara ya Afrika, Amerika, Asia na Ulaya.

 
Nishani hiyo alivishwa na Rais wa Baraza hilo Brig Gen Herve Piccilliro  kutoka Ufarasa mbele ya wajumbe takribani 400 waliohudhuria Mkutano huo kutoka pande zote duniani. 

Kanali Bakari anakuwa ni Mtanzania pekee kupata nishani ya pili ya utendaji bora katika baraza hilo. Mwaka 2008 aliwahi kutunukiwa  nishani iitwayo Grand Knight nchini Suriname mjini Paramaribo kufuatia juhudi zake za kukuza vipaji vya michezo kupitia kituo cha Twalipo Youth Sports ambacho alikianzisha.

Baraza la michezo ya Majeshi hutunuku nishani kwa yeyote ambaye kwa matendo yake ametekeleza malengo ya CISM na kwa utendaji wake amechangia maendeleo ya michezo kwa majeshi ya nchi wanachama.

Baadhi ya Wanajeshi waliotunikiwa nishani Pamoja na Kanali Bakari katika madaraja mbalimbali ni Pamoja na Maj Gen  Katirima Manoni Phinehas (Uganda),  Kanali  Moussa Moise Keita (GUINEA), Mteule Bongseok Kim (USA), Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Peru  Luteni Jenerali  David Guillermo Ojeda Parra, Kapteni wa Wanamaji  Spyridon Andriopoulos (UGIRIKI),  Meja Jenerali Grancisco Javier Costa Gallegos (PERU),  Luteni Kanali  Lars Gerhardsson (SWEDEN), Luteni Kanali  Jan Van den Dool (UHOLANZI). 

Aidha, mkutano huo pia uliazimia  kuendelea  kusimamia msimamo wa kutoingilia  mgogoro unaoendelea kati ya nchi mbili wanachama wa Baraza hilo ambazo ni Urusi na Ukraine, kufuatia nchi ya Ukraine  kutoa  shinikizo kwa baraza hilo ili iifungie na kuitenga nchi ya Urusi kushiriki kwenye shughuli za baraza hilo kutokana na mgogoro huo.

Akiwasilisha  maamuzi ya Bodi ya Wakurugenzi Rais wa CISM Brigedia  Jenerali Herve Piccilliro alisema  Kwa mujibu wa kanuni  baraza hilo sio chombo cha kisiasa, halitakuwa upande wowote na hivyo haitaifungia wala kuitenga Urusi au kuifuta uanachama, Isipokuwa  nchi wanachama zipo huru kutoshirikiana na Urusi kama sehemu ya maagizo ya nchi zao. 

 
Katika hatua nyingine mkutano huo ulifanya chaguzi kwa nafasi za Rais , Katibu Mkuu na Mhazini.
 
Katika nafasi ya Rais aliyekuwa anagombea nafasi hiyo akiwa ni mgombea pekee na ambaye alikuwa madarakani Brigedia Jenerali  Herve Piccilliro alishindwa kutetea nafasi yake baada ya kupata kura 27 za Ndio, 22 za Hapana na 16 za kutofanya uamuzi wa kuchagua ( abstention). Hivyo hakuchaguliwa kutokana na kushindwa kupata zaidi ya nusu ya kura zote ( absolute majority).  

Kwa matokeo hayo nafasi ya Rais wa baraza hilo imeshikiliwa kwa muda na Rais wa Bara la  Ulaya Kanali Dirk Schwedi hadi uchaguzi ujao mwakani.

Katika nafasi ya Katibu  Mkuu mgombea pekee Kapteni wa Wanamaji Recchia wa Italia  alichaguliwa na kwa nafasi ya Mhazini Kanali Sven Serre  wa Ubelgiji alichaguliwa. 

Aidha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza hilo aliyemaliza muda wake Kanali Dorah Mamby Koita wa  Guinea alichaguliwa kuwa Balozi maalum wa Baraza hilo. 

“CISM” ( International Military Sports Council/ Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani ni moja kati ya Shirikisho kubwa duniani linalojishughulisha na michezo anuai (multdisplinary).

Baraza hilo linaloundwa na majeshi ya nchi wanachama  140 Tanzania ikiwemo.
Dhima Kuu ya Shirikisho hilo ni kutumia michezo kama njia na zana ya kueneza amani duniani badala ya vita. 

Hivyo kupitia Shirikisho hilo nchi wanachama zinaaswa na kupewa wito kuwa yale waliyokuwa wanayafanya katika uwanja wa vita sasa wayafanye katika viwanja vya michezo.

Shirikisho hilo huandaa  mashindano zaidi ya 20 ya dunia kwa Mwaka mashindano ya Mabara na kikanda katika michezo zaidi ya 30.

Shirikisho limekuwa likisisitiza  Masuala yahusiyo uongozi,  uamuzi, ualimu,  tiba na katazo la matumizi ya nguvu za kusisimua misuli katika michezo.

Aidha, kama Mkurugenzi wa baraza hilo Kanali Bakari aliwasilisha mada mbalimbali kuhusu utekelezaji wa majukumu yake.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here