Waziri wa nishati nchini, Mh January Makamba ameahidi kufanya ziara mwezi huu April 2022 mkoani Iringa kukutana na wafanyabiashara wa nguzo za umeme wa nyanda za juu kusini ili kufikia makubaliano na kuondoa changamoto iliyojitokeza juu ya biashara hiyo ya nguzo za umeme.
Akijibu baadhi ya hoja za wabunge waliochangia katika hotuba ya waziri mkuu wiki hii, Mh Makamba amesema yupo tayari kukutana na wadau husika wa katika biashara ya nguzo za umeme.
Katika hatua nyingine, Makamba amesema kupanda kwa bei ya mafuta kumetokana na nchi zinazozalisha mafuta kupandisha bei ya uuzaji wa bidhaa hiyo hali inayopelekea bei kupanda katika miezi 10 iliyopita.
Amesema serikali itatimiza ndoto ya muda mrefu ya kuwa na hifadhi ya Kimkakati ya Taifa ya mafuta mapema mwaka huu ambapo kwa sasa serikali inakamilisha kanuni za kuiwezesha kukamilika kwa hifadhi hiyo.
Ameongeza kuwa serikali imepata washirika wa uwekezaji wa miundombinu ya ushushaji na uhifadhi wa mafuta ili kuwezesha hifadhi hiyo kufanya kazi.
Makamba amefungua milango kwa Watanzania wenye taarifa za maeneo yanapoweza kupatikana kwa mafuta kwa bei rahisi kufika katika ofisi za wizara ili kuweza kusaidia upatikanaji wa bidhaa hiyo.
Ikumbukwe kuwa mapema wiki wabunge mbalimbali kutoka nyanda za juu kusini akiwemo mbunge wa Mafinga Mjini, Mh. Cosato Chumi pamoja na Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Dkt Ritta Kabati kuonesha wasiwasi wao kuhusu uingizwaji wa nguzo za umeme kutoka nje ya nchi kwa kile kilichodaiwa kutokana na ubora wa nguzo hapa nchini.
Awali wabunge hao waliita mpango huo kuwa ni wa kufifisha uchumi wa mikoa ya nyanda za juu kusini unaotegemea zaidi mazao ya misitu.