Home LOCAL WANANCHI EPUKENI KUJENGA MAENEO HATARISHI

WANANCHI EPUKENI KUJENGA MAENEO HATARISHI

 Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Kaspar Mmuya akiongoza kikao cha Baraza la Usimamizi wa Maafa kilichohusisha Mkatibu Wakuu wa Wizara ambazo ni wadau wa usimamizi wa maafa Aprili 04, 022 katika Ukumbi wa ofisi hiyo Dodoma

Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Bw. Samwel Mbuya akichangia hoja wakati wa kikao hicho.

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Usimamizi wa Maafa wakifuatilia kikao hicho katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Aprili 04, 2022 Dodoma.

Afisa Elimu Mkuu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Bi. Wengi Mchuchary akichangia hoja wakati wa kikao hicho na (wa pili kulia) ni Afisa Misitu Mkuu kutoka TAMISEMI Bw. Rogasian Lukoa akifuatilia kikao hicho.

Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Michael Mumanga akifafanua jambo katika kikao cha Baraza hilo kilichofanyika katika ofisi hiyo Aprili 04, 2022 Dodoma.

Na: Mwandishi Wetu-Dodoma

Serikali imewataka wananchi kuepuka kujenga katika maeneo hatarishi yanayoweza kusababisha maafa kama vifo, uharibifu wa miundo mbinu na mazingira nchini.

Hayo yalisemwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Bw. Kaspar Mmuya wakati wa kikao cha Baraza la Usimamizi wa Maafa kilichokutanisha Makatibu Wakuu wa Wizara ambazo ni wadau wa usimamizi wa maafa na wataalam katika ukumbi wa Ofisi hiyo Jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kuwa ipo haja ya wananchi kupewa elimu kupitia wataalamu mbalimbali kuhusu dhana ya usiammaizi wa maafa na namna ya kuzuia madhara ya maafa au kuchukua hatua ya kujiokoa pindi yanapotokea.

“Tunahimiza tufuate maelekezo ya wataalamu kwa kutojenga kwenye maeneo ambayo hayafai hasa ya mabondeni, kujiepusha na kulima maeneo ya vyanzo vya maji na wafugaji kutokuwa na mifugo mingi ambayo anashindwa kuihudumia hatimaye tatizo likitokea la ukame anashindwa kuwapa huduma bora,”alisema Bw. Mmuya.

Pia akizungumzia kuhusu hali ya hewa aliwahimiza wakulima nchini kuzingatia utabiri wa hali ya hewa ambao umekuwa ukitolewa na wataalam ili kujua mazao rafiki ya kulima kwa msimu husika.

“Tuangalie mabadiliko ya hali ya hewa tuweze kulima kulingana na hali ya hewa na elimu hii itatolewa kwa wakulima kama kipindi cha mvua nyingi tunatakiwa kulima nini na wakati wa mvua chache tulime nini elimu hii itatolewa maeneo yote,”alieleza.

Aidha kuhusu sera alibainisha kwamba ofisi hiyo kama wasimamizi wa sera na wasimamizi wa maduhuli katika kila wizara hazina budi kuweka bajeti itakayosaidia  kukabili changamoto zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

“Kwa sisi  wasimamizi wa sera na waduhuli katika kila wizara kujaribu kuweka bajeti kila wizara ili tatizo linapojitokeza tuwe na mpango wa muda mfupi kutekeleza changamoto zinatokana na mabadiliko ya hali ya hewa,” alibainisha Bw. Mmuya.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Michael Mumanga alisisitiza sekta mbalimbali zinazohusika na uhifadhi wa chakula na uokoaji kuweka mikakati thabiti itakayosaidia kudhibiti maafa na kuyakabili pindi yanapojitokeza.

MWISO

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

 

Previous articleYASEMAVYO MAGAZETI ASUBUHI YA LEO JUMANNE APRIL 5-2022
Next articleRAIS SAMIA ASISITIZA USHIRIKIANO NA VYAMA VYOTE VYA SIASA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here