Home BUSINESS VISIMA VYA NISHATI YA JOTOARDHI KUANZA KUCHORONGWA SONGWE

VISIMA VYA NISHATI YA JOTOARDHI KUANZA KUCHORONGWA SONGWE

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati , Eng. Felchesmi Mramba (katikati) akitazama maji ya moto yanayotoka ardhini  katika Kijiji cha Nanyala wilayani Mbozi mkoani Songwe ikiwa ni moja ya ishara za uwepo wa nishati ya Jotoardhi katika eneo hilo. Kulia kwake ni Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Mathew Mwangomba na kushoto kwake ni Mhandisi Shakiru Idrissa, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara kutoka TGDC

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba (Wa Sita kushoto) na Wafanyakazi wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), TANESCO pamoja na wakazi wa Kijiji cha Nanyala katika eneo ambalo utafanyika uchorongaji wa kisima cha  Jotoardhi ambapo mategemeo yake ni kupata Megawati 5 – 38 za Umeme wa Jotoardhi.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati , Eng. Felchesmi Mramba akisisitiza jambo wakati wa  ziara yake katika eneo la uendelezaji wa Jotoardhi mkoani Songwe. Kulia kwake ni Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Mathew Mwangomba na kushoto kwake ni Mhandisi Shakiru Idrissa, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara kutoka TGDC.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati , Eng. Felchesmi Mramba (katikati) akikagua eneo lenye nishati ya Jotoardhi katika Kijiji cha Nanyala wilayani Mbozi mkoani Songwe. Kulia kwake ni Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Mathew Mwangomba na kushoto kwake ni Mhandisi Shakiru Idrissa, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara kutoka TGDC.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati , Eng. Felchesmi Mramba (wa Pili kulia) akipata maelezo kutoka kwa Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Mathew Mwangomba (wa Pili kushoto)  kuhusu kifaa cha ukusanyaji wa taarifa za Jotoardhi kilichofungwa katika eneo lenye nishati ya Jotoardhi katika Kijiji cha Nanyala wilayani Mbozi, Mkoa wa Songwe. Wa kwanza kulia ni Mhandisi Shakiru Idrissa, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara kutoka TGDC.

Imeelezwa kuwa, Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) kuanzia mwezi Mei mwaka huu itaanza kuchoronga visima vifupi vya utafiti katika mradi wa Jotoardhi Songwe, vitakavyosaidia kupata taarifa za uhakika za kisayansi zitakazowezesha mradi huo kuanza kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 5 ifikapo mwaka 2023.

Hayo yalisemwa tarehe 15 Aprili, 2022 wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba katika eneo utakapotekelezwa mradi huo wa Jotoardhi katika Kijiji cha Nanyala wilayani Mbozi, Mkoa wa Songwe.

Mhandisi Mramba alieleza kuwa, lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kujionea hali ya eneo hilo, hatua zilizofikiwa hadi sasa za uendelezaji wa rasilimali hiyo ya Jotoardhi pamoja na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa ili kuweza kupata umeme kutokana na nishati hiyo.

Alisema kuwa, Serikali imejikita katika kuendeleza nishati Jadidifu ambazo ni endelevu, salama na rafiki wa Mazingira kama vile Jotordhi ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na uhakika wa uzalishaji umeme nchini kwani nishati nyingine kama vile Gesi Asilia ambayo inazalisha umeme kwa kiasi kikubwa kwa sasa nchini huwa inaisha tofauti na nishati jadidifu kama ya Jotoardhi.

Aidha, alielekeza kuwa, wakati TGDC ikiwa kwenye mpango wa kuanza kuchoronga visima vya majaribio na vya kuzalisha mvuke, wanapaswa kuwa na hatimiliki ya eneo hilo ili kuwa na uhakika na eneo hilo ambalo lina manufaa makubwa kwa nchi.

Vilevile aliipongeza TGDC kwa kuwa tayari imeanza kujipanga na uendelezaji wa eneo la mradi ikiwemo uwepo wa viwanda mbalimbali kama vile vinavyohitaji Joto na Majimoto ili kutekeleza za uzalishaji na hivyo aliwaasa wananchi wa Kijiji hicho cha Nanyala kuendelea kutunza eneo hilo litakalokuwa na manufaa.

Awali, Kaimu Meneja Mkuu wa TGDC, Mhandisi Mathew Mwangomba, alimweleza Katibu Mkuu kuwa,  mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2018 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2023/24  ukiwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 5 hadi 38.

Alisema kuwa, pamoja na kujipanga na kuanza kazi ya kuchoronga visima, TGDC inaendelea na utekelezaji wa miradi ya matumizi mengine katika eneo la mradi ikiwemo kuongeza thamani ya mazao ya mifugo ambapo kutajengwa mabwawa ya kufugia Samaki pamoja na teknolojia ya kutotolesha vifaranga vya kuku kwa kutumia Jotoardhi.

Aliongeza kuwa, miradi mingine inayoendelea kutekelezwa kutokana na uwepo wa nishati ya Jotoardhi ni pamoja na uendelezaji wa kilimo ambapo kutajengwa nyumba kitalu kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kama kukausha mazao kwa kutumia joto na kuboresha vivutio vya utalii  vinavyopatikana katika maeneo ya Jotoardhi kama vile bwawa la kuogelea la majimoto.

Tanzania ina uwezo wa kuzalisha umeme wa Jotoardhi usiopungua megawati 5000 zinazopatikana ndani ya mikoa 16 nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here