Tafiti zimeonesha kuwa vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Malaria vimepungua kwa asilimia 70 huku watu ambao wapo kwenye hatari ya kuambukizwa ni asilimia 94 ndani ya mwaka.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha ufuatiliaji wa tathmini ya udhibiti wa Malaria Dkt. Sijenunu Aron alipokuwa akitoa mada ya hali ya Maralia nchini katika semina ya waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya siku ya Malaria ambapo hufanyika kila Aprili 25 kila mwaka duniani.
Dkt. Aron amesema takwimu za dunia za mwaka 2021, zinaonesha kuwa kwa mwaka 2020 kulikuwa na ongezeko la wagonjwa wanaokadiriwa kufikia milioni 241 katika nchi 85 zenye ugonjwa huo kutoka wagonjwa milioni 227 huku vifo vikiongezeka hadi kufikia vifo 627,000 kukiwa na ongezeko la vifo 69,000 sawa na asilimia 12 ikilinganishwa na vifo 558,000 kwa mwaka 2019.
“Inakadiriwa vifo 47,000 sawa na asilimia 68 ya vifo 69,000 viliovyoongezeka vimechangiwa na uwepo wa ugonjwa wa Covid-19,” alisema.
Aidha, Dkt. Aron amesema pamoja na kupungua kwa Malaria hadi kufikia asilimia 7.5 mwaka 2017, bado asilimia 94 ya watanzania wako katika hatari ya kupata maambukizi ya ugojwa huo.
Alisema utafiti inaonesha kuwa maambukizi kwa watoto wa shule za msingi yamepungua kutoka asilimia 21.6 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 11.2 mwaka 2021.
Dkt. Aron alisema idadi ya wagonjwa imepunguwa kwa asilimia 53 kwa kila wagonjwa 1000 kutoka wagonjwa 162 hadi kufikia wagonjwa 76.
Mikoa ambayo ina kiwango kikubwa cha Malaria ni Lindi, Mtwara, Pwani, Ruvuma, Tanga na Tabora wakati ile yenye kiwango kidogo ni Kilimanjaro, Manyara, Arusha, Dodoma, Iringa, Singida na Njombe.
Dk. Aron alisema wagonjwa waliolazwa kutokana na Malaria imepungua kwa asilimia 32 kutoka wagonjwa 307,588 mwaka 2017 hadi 209,888 mwaka 2021 wakati vifo vimepungua kwa asilimia 70 kati ya vifo 100,000 kutoka vifo 6,311 mwaka 2015 hadi 1,909 mwaka 2021.
Serikali inatekeleza afua nne za kupambana na mbu wanaoambukiza ugonjwa huo sambamba na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba, vitendanishi na dawa kwa zaidi ya asilimia 90 katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya.