Home LOCAL UTEKELEZAJI MIRADI YA MAJI KUPITIA FEDHA ZA UVIKO-19 WASHIKA KASI KATIKA WILAYA...

UTEKELEZAJI MIRADI YA MAJI KUPITIA FEDHA ZA UVIKO-19 WASHIKA KASI KATIKA WILAYA YA NACHINGWEA

Mhandisi Milembe Lukenza ambaye ni Msimamizi wa mradi wa Maji Mchangani(kulia) akibeba tofali kwa ajili ya kusaidia mafundi wanaoendelea na ujenzi wa tanki la maji.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA)Mkoa wa Lindi Mhandisi Muhibu Lubasa akitoa ufafanuzi kuhusu miradi ya maji inayotekelezwa kwa fedha za UVIKO-19 inavyotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo ambapo jumla ya Sh.bilioni 2.6 ambazo zinatekeleza miradi sita.


Tanki la maji ambalo ujenzi wake bado unaendelea linavyoonekana kwa chini .Tanki hilo linajengwa katika mradi wa maji Mchangani.


Mhandisi Milembe Lukenza ambaye ni Msimamizi wa mradi wa Maji Mchangani(kulia) akishiriki katika na baadhi ya mafundi kwenye ujenzi wa tanki la maji ambalo ujenzi wake bado unaendelea.


Mhandisi Sultan Ndoliwa ambaye ni Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nachingwea akisisitiza jambo wakati akielezea mradi wa maji Mchangani.


Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi Mhandisi Sultan Ndoliwa akitoa maelekezo kuhusu namna wanavyotekeleza ujenzi wa tanki la maji katika mradi wa maji Mchangani.


Mhandisi Sultan Ndoliwa ambaye ni Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nachingwea akipanda kwenye tanki ambalo ujenzi wake bado unaendelea katika eneo la Mchangani.



Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA) Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi Mhandisi Sultan Ndoliwa (kulia) akiwa na Mhandisi Milembe Lukenza ambaye ni Msimamizi wa mradi wa Maji Mchangani (kushoto)wakijadiliana jambo baada kukagua mradi huo wa maji unaotekelezwa kwa fedha za UVIKO-19.

Mafundi wakiendelea na ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita 100,000 ambalo lipo kwenye mradi wa maji Mchangani katika Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.Mradi huo unatekelezwa kwa kutumia fedha za Ustawi maarufu fedha za UVIKO-19 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa lengo la kutatua changamoto ya upatikanaji maji maeneo ya vijijini.

Na: Mwandishi wetu, NACHINGWEA

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA)Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi umesema kupatikana kwa miradi ya maji inayotekelezwa kwa fedha za UVIKO-19 ambazo zimetolewa na Serikali ya Awamu ya Sita itakwenda kuongeza kiwango cha upatikanaji maji ndani ya wilaya hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nachingwea Sultan Ndoliwa amesema Wilaya hiyo kwa sasa inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji mitano ukiwemo mradi wa maji Mchangani ambao unatekelezwa kwa fedha za UVIKO-19.

“Hapa tuko kwenye Kijiji cha Mchangani na mradi huu wa maji ambao tunaotekeleza unagharimu sh.milioni 475 na utakuwa na vituo vinane vya kuchotea maji na una mtandao wa bomba kilometa 14.5.Mradi huu unakwenda kunufaisha watu  3,682 utakapokamilika,”amesema.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha ili kufanikisha miradi hii kwa lengo la kuondoa changamoto ya upatikanaji maji maeneo ya vijijini, kwetu tunasema miradi hii inayotekelezwa kwa fedha za UVIKO-19 imekuja wakati muafaka, kwani tunakwenda kutatua changamoto ya uhaba wa maji kwa wananchi wa Wilaya yetu ya Nachingwea.”

Aidha amesema  mradi mwingine wanaoutekeleza kwa fedha za ustawi ni mradi wa maji katika kijiji cha Lionjo unaogharimu fedha Sh.milioni 309 na utakapokamilika utahudumia watu 3546 , kwa sasa uko hatua za awali na utakuwa na vituo tisa vya kuchotea maji.

“Mradi mwingine ambao RUWASA Wilaya ya Nachingwea tunautekeleza ni mradi wa maji katika Kijiji cha  Ruponda,Namanga,Mwanyamala na Nyangawa ambao unagharimu  Sh.milioni 761 na utakapokamilika utahudumia watu watu 6220.

Mhandisi Ndoliwa amesema kwa ujumla miradi hiyo ya maji ikiwemo inayotekelezwa kwa fedha za UVIKO-19 ikikamilika itaongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia ya sasa 62 hadi asilimia 73 na jumla ya fedha zote zinazotekeleza miradi ni Sh.bilioni 1.6.

Kuhusu kufukia asilimia 85 ya upatikanaji wa maji ifikapo mwaka 2025, amesema baada ya kukamilisha miradi hiyo pamoja na miradi  mingine minne ambayo wanatarajia kuanza kuitekeleza watafikia asilimia hiyo.

Alipoulizwa kuhusu vyanzo vya maji vilivyopo kwenye Wilaya hiyo, amesema wanategemea visima virefu lakini pia kuna vyanzo vya maji ya  chemchem kupitia bomba ku.

Kwa upande wake Mhandisi Milembe Lukenza ambaye ni Msimamizi wa mradi wa maji Mchangani unaotekelezwa kwa fedha za UVIKO-19 amesema kuwa anamshukuru Rais Samia kwa kuonesha upendo wake kwa wananchi wa wilaya ya Nachingwea kwa kuamua kuwapelekea mradi huo wa maji.

Ametumia nafasi hiyo kutoa rai ka wakandarasi wanawake wote ambao wamekuwa sehemu ya kusimamia miradi ya maji inayotokana na fedha hizo wahakikishe wanatekeleza majukumu yao kwa weledi, ufanisi na uaminifu mkubwa na kwamba wanawake wanayo nafasi ya kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo ya Taifa la Tanzania.

Awali Mhandisi wa Mkandarasi wa Kampuni ya Kharton Traders Limited Daud Omari  ambaye ni Msimamizi wa ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita 100,000 katika mradi huo amesema wanamshukuru Rais Samia kwa kuwakumbuka wakandarasi wazawa katika kujenga miradi hiyo ya maji.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa wa Kijiji cha Mchangani wamesema wanatoa shukrani kwa RUWASA pamoja na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia kwa kuamua kutatua changamoto ya maji katika kijiji hicho.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi huu wa maji wilayani Nachingwea na hasa katika Kijiji cha Mchangani , kupata mradi huu maana yake ni moja tu tunakwenda kuondokana na adha ya kufuata maji umbali mrefu, hata wanafunzi watakuwa wanawahi shule kwani watakuwa wakichota maji karibu tofauti na ilivyo sasa.”

Mwisho.

Imeandaliwa, Na: Saidi Mwishehe, Michuzi TV-Nachingwea

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here