Home LOCAL TMA YATOA UFAFANUZI ATHARI MABADILIKO TABIA NCHI ILIVYOATHIRI MIFUMO YA HALI YA...

TMA YATOA UFAFANUZI ATHARI MABADILIKO TABIA NCHI ILIVYOATHIRI MIFUMO YA HALI YA HEWA.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania-TMA Dkt Agnes Kijazi akizungumza na wananahabri jijini Dar es salaam akielezea mwenendo wa athari za mabadiliko ya Tabia nchi katika mifumo ya hali ya hewa na mwenendo wa mvua za masika mwaka huu.


Mratibu wa maafa Ofisi ya waziri Mkuu Idara ya usimamizi wa maafa Khowe Malegeri akizungumza nanma ofisi hiyo itakavyokabiliana na maafa yanayoweza kujitokeza.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania-TMA imewashauri wakulima katika kipindi kilichosalia cha msimu wa masika mwaka huu,kuzingatia matumizi ya mbinu na teknolojia za kilimo himilivu za kuhifadhi maji na unyevunyevu wa udongo pamoja na kuzingatia maelekezo ya maafisa ugani kwenye maeneo yao.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt Agnes Kijazi wakati akizungumzia mwenendo wa athari za mabadiliko ya Tabia nchi katika mifumo ya hali ya hewa na mwenendo wa mvua za masika mwaka huu ambapo amesema mvua inatarajiwa kuwa ya chini ya wastani hadi wastani.

Dkt Kijazi amesema kutokana na kujitokeza kwa matukio ya vimbunga katika bahari ya Hindi eneo la Rasi ya Msumbiji kusini kumesababisha kuwepo na vipindi virefu vya ukavu vilivyojitokeza kipindi cha mwezi machi hususani kwa maeneo ya pwani ya Kaskazini na Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki ambapo maeneo hayo yamepata mvua chache.

‘Vilevile yamejitokeza mabadiliko ya muda mfupi ya joto la bahari katika eneo la Pwani ya Afrika Mashariki na eneo la mashariki mwa bahari ya Hindi.Mabadiliko hayo ya muda mfupi ya joto la bahari ambayo ni nadra kutokea kutokana na tabia ya bahari kutunza joto au baridi kwa muda mrefu yamesababishwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi’amesema Dkt Kijazi

Kuhusu athari zinazoweza zinazotarajiwa Dkt Kijazi amesema kunatarajiwa kuwepo kwa upungufu wa unyevu katika udongo ambapo hali hiyo inaweza kuathiri ukuaji wa mazao,upatikanaji wa malisho kwa ajili ya mifugo na wanyamapori pia upo uwezekano wa kuongezeka kwa athari za magonjwa ya kuambukiza,hususani yatokanayo na maji yasiyosalama.

Kwa upande wake Mratibu wa maafa Ofisi ya waziri Mkuu Idara ya usimamizi wa maafa Khowe Malegeri amezielekeza sekta zote zinazohusiana na kilimo mifugo na miundombinu kuchukua hatua stahiki ili kurejesha hali inayopelekea kuwepo kwa upungufu wa chakula na kudhurika kwa mifugo.

Juma Makandi ni mdau katika sekta ya Kilimo amesema watahakikisha wanafanyia utekelezaji taarifa hizo ambazo zimetolewa na TMA huku akiwashauri wakulima kutumia njia himilivu zinazoweza kutunza unyevu na maji.

Hata hivyo wananchi wametakiwa kuendelea kuzingatia taarifa za hali ya hewa zilizotolewa na zitakazotolewa na Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania ikiwa ni pamoja na kutafuta,kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika ili kuweza kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here