Home LOCAL TANZANIA, UAE ZASAINI MAKUBALIANO KUIMARISHA USHIRIKIANO

TANZANIA, UAE ZASAINI MAKUBALIANO KUIMARISHA USHIRIKIANO

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha hotuba yake katika Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Tanzania na UAE leo Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Nchi wa UAE, Shakhbout bin Nahyan Al Nahyan akiwasilisha hotuba yake katika Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Tanzania na UAE uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akibadilisha mkataba wa makubaliano na Waziri wa Nchi wa UAE, Shakhbout bin Nahyan Al Nahyan mara baaya ya wawili hao kumaliza kusaini mikataba hiyo.
 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akibadilisha mkataba wa makubaliano na Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini Mhe. Khalifa Abdulrahman Mohamed Al-Marzooqi mara baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo katika kikao cha ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
 

Mawaziri, Mabalozi na Makatibu wakuu wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa mkutano

Na: Mwandishi Wetu, Dar

Serikali ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E), zimesaini Makubaliano ya Tume ya Kudumu ya Pamoja katika nyanja za forodha, elimu, kilimo, nishati, mawasiliano, ulinzi na usalama.
 
Makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Nchi wa UAE, Shakhbout bin Nahyan Al Nahyan katika Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Tanzania na UAE leo Jijini Dar es Salaam
 
Akizungumza katika hafla hiyo iliyotanguliwa na kikao cha Makatibu Wakuu, Waziri Mulamula amesema kusainiwa kwa makubaliano hayo ni ishara tosha ya kunaimarika zaidi kwa ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili.
 
“Kusainiwa kwa makubaliano hayo kunatoa fursa kati ya Serikali ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu kuendeleza biashara na uwekezaji ,” amesema Balozi Mulamula
 
Kwa upande wake Waziri wa nchi wa UAE Mhe. Sheikh Shakhboot Nahyan Al Nahyan amesema ni faraja kwa kwa kusainiwa kwa makubaliano hayo kwani wamesubiri kwa muda, na kilicho bakia ni utekelezaji wa maeneo waliyokubaliana kwa maslahi ya mataifa yote.
 
“Natumaini yale tuliyozielekeza chemba za biashara za pande zote mbili kuhakikisha kuwa zinashirikiana zaidi katika kuboresha zaidi mazingira ya bishara na uwekezaji kwa maslahi ya pande zote mbili,” amesema Mhe. Al Nahyan
 
“Baada ya kusainiwa kwa makubaliano haya tumedhamiria kuanza kuongeza maeneo ya ushirikiano baina yetu katika sekta za elimu, nishati, kilimo, biashara na mawasiliano,”amesema Al Nahyan.
 
Awali, akiwasilisha hotuba yeke, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab amesema kusainiwa kwa makubaliano ya Tume ya Kudumu ya pamoja kati ya Tanzania na UAE ni wazi kuwa ushirikiano baina ya Tanzania na UAE utazidi kuimarika zaidi.
 
“Pamoja na mambo mengine, kikao cha Makatibu Wakuu tumejadili na kukubaliana kuongeza ushirikiano katika nyanja za biashara na uwekezaji, mawasiliano, usafirishaji pamoja na ulinzi na usalama……kusainiwa kwa makubaliano haya kunaakisi ishara nzuri ya kuendeleza ushirikiano baina yetu,” amesema Balozi Fatma
 
Naye Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) Balozi Mohammed Mtonga amebainisha fursa mbalimbali zinazopatika katika Falme za Kiarabu ikiwa ni pamoja na masoko ya matunda, nyama na korosho.
 
Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Tanzania na UAE ulifanyika mwaka 2016

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here