Home LOCAL TAKUKURU MKOA WA GEITA YABAINI MAPUNGUFU KWENYE MIRADI 15.

TAKUKURU MKOA WA GEITA YABAINI MAPUNGUFU KWENYE MIRADI 15.

Na: Costantine James, Geita.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Geita, imebaini mapungufu katika  miradi 15 yenye thamani ya Sh. Bilioni 18.3 haijazingatia vigezo na mashariti yaliyoainishwa kwenye michoro na Tathimini ya Ujenzi (BOQ) wa miradi hiyo.

 Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Takukuru mkoani Geita, Leonidas Felix wakati akitoa taarifa ya ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2022, kulenga kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma.

Alisema miradi hiyo ni kati ya miradi 19 ya maendeleo iliyofuatiliwa na kukaguliwa ndani ya kipindi hicho katika sekta za afya, elimu, ujenzi, maji na kilimo yenye thamani ya Sh bilioni 18.67 kwa mjibu wa mikataba ya miradi husika.

Leonidas alieleza, miradi hiyo yenye mapungufu imebainika kukosa usimamizi thabiti kutoka kwa wataalamu wa halmashauri pamoja na baadhi ya mafundi walioshinda zabuni za ujenzi kutokuonekana katika eneo la mradi.

“Wahandisi wamewaacha mafundi wasaidizi pasipo usimamizi wala maelekezo eneo la ujenzi. Baada ya ufuatiliaji huu wahusika walishauriwa namna bora ya kuboresha utekelezaji wa miradi hiyo kupitia vikao kazi.

“Miradi minne katika sekta ya elimu yenye thamani ya Sh. milioni 340 ilionekana kuwa na viasharia vya ufujaji na ubadhirifu wa fedha hivyo uchunguzi umeanzishwa na unaendelea alisema Leonidas Felix Mkuu wa Takukuru mkoa wa Geita”.

Aidha aliweka wazi uchunguzi umefanyika juu ya miradi ya Madarasa kwa Fedha za Kukabiliana na Madhara ya Janga la Korona (TCRP) na watuhumiwa wameagizwa kufanya marejesho ya fedha zote zilizofujwa.

Leonidas alisema wanaendelea na upembuzi wa mifumo na viasharia vya rushwa ya ngono katika sekta ya elimu, afya na madini na tayari maadhimio yamefikiwa namna bora ya kudhibiti mianya ya rushwa hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here