Wekundu wa Msimbazi timu ya Simba SC imeibuka kidedea kwa kuichapa timu ya Gendarmerie ya nchini Niger kwa jumla ya magoli 4-0 katika Dimba la Mkapa Jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kuingia robo fainali ya Kombe la Shirikisho Africa.
Katika mchezo huo kiungo wa Simba Sadio Kannote alifungua pazia la magoli kwa kuipatia timu yake bao la kuongoza dakika 63 kufuatia pasi safi kutoka kwa Kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Bernard Morison.
Timu ya Simba iliendelea kucheza kwa kazi na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara kwa kulisakama lango la Gendarmerie ambapo dakika ya 68 Mshambuliaji wa timu hiyo raia wa Congo Chiss Mugalu alipachika bao la pili akimalizia Mpira uliopigwa na Kibu Dennis alieingia kuchukua nafasi ya Lally Bwalya ikiwa ni tofauti ya dakika 5 toka goli la kwanza kufungwa.
Mnamo dakika ya 79 Criss Mugalu tena alipachika bao la tatu akifanya kazi kubwa ya kumalizia Mpira uliombabatiza Beki huku Mugalu akijituma kwa kuamka chini na kurudisha tena golini.
Mashambulizi ya Simba yalizidi kuichanganya timu ya Gendarmerie ambapo tipa wa timu hiyo alijikuta akiusindikiza Mpira nyavuni kwa kushindwa kuudhibiti Mpira alipokuwa amerudishiwa na Beki wake.
Kwa matokeo hayo timu ya Simba SC inaungana na timu ya Berkane FC ya Morocco kwenda kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.