Home LOCAL SHILINGI BILIONI 1.3 KUMALIZA KERO YA MAJI KWA WANANCHI WA MITUMBATI NA...

SHILINGI BILIONI 1.3 KUMALIZA KERO YA MAJI KWA WANANCHI WA MITUMBATI NA NAMIJATI

Tenki la kuhifadhia maji linalojengwa na wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)katika kijiji cha Mitumbati kata ya Mkonona ambalo likikamilika litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita 100,000 za maji.

Meneja wa Ruwasa wilayani Nanyumbu Mhandisi Simon Mchucha aliyevaa kapelo mbele,akiwaongoza viongozi wa Serikali ya kijiji cha Mitumbati kuangalia ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji linalojengwa kupitia mradi wa maji wa Mitumbati-Chilunda.


Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mitumbati wilayani Nanyumbu Hussen Salehe wa tatu kushoto na Meneja wa Ruwasa wilaya ya Nanyumbu Mhandisi Simon Mchucha wa pili kushoto wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukagua ujenzi wa tenki la maji linalojengwa katika kijiji hicho.


Meneja wa Ruwasa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwarwa Mhandisi Simon Mchucha akiwaongoza baadhi ya viongozi wa Serikali ya kijiji cha Mitumbati kata ya Mkonona wilayani humu kukagua ujenzi wa tenki la maji ambalo likikamilika litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita 100,000 za maji.


Tenki la kuhifadhi maji linalojengwa katika kijiji cha Namijati na Wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)likiwa katika hatua za mwisho kukamilika.

Meneja wa Ruwasa wilayani Nanyumbu Mhandisi Simon Mchucha kushoto,akikagua moja kati ya vituo vya kuchotea maji katika kijiji cha Namijati wilayani humo,katikati ni Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Chuachua Rashid.
 
Na: Muhidin Amri, Nanyumbu

WAKAZI wa kijiji cha Mitumbati na Namijati kata ya Mkonona wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara,wameishukuru serikali kwa kuwajengea mradi mkubwa wa maji unaotarajiwa kumaliza kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi hao walisema, kuanza kwa ujenzi wa mradi huo kumewapa matumaini makubwa ya kumalizika kwa kero ya maji,iliyowafanya kutumia maji ya visima vidogo vya asili na maji ya mto Ruvuma.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mitumbati Hussen Saleh alisema,kujengwa kwa mradi huo ni faraja kubwa kwao kwa kuwa utamaliza kilio cha muda mrefu na umeleta matumaini mapya ya kutumia maji ya bomba kama ilivyo katika maeneo mengine hapa nchini.

Alisema, kwa muda mrefu wakazi wa kijiji ca Mitumbati wanatumia maji ya kisima cha asili ambacho hakitosheleza mahitaji yao na maji ya mto Makanya ambayo sio safi na salama jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.

Aidha,ameiomba wizara ya maji kupitia wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilayani humo, kufanya maandalizi ya kusambaza mabomba ya maji kwenda kwa wananchi ili iwe rahisi kuchangia gharama na kuepusha migogoro badala ya kutegemea vituo vya kuchotea maji.

Alisema,wananchi wa kijiji hicho wana hamu kubwa kuona mradi unakamilika haraka na wameshaanza kuweka fedha kidogo kidogo kwa ajili ya kuunganishiwa huduma ya maji kwenye nyumba zao.

Mkazi wa kijiji hicho Sofia Kanyenda alisema, mradi huo utakapokamilika utasaidia kumaliza changamoto ya kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji muda ambao wangeweza kuutumia kufanya shughuli nyingine za maendeleo.

Naye Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Namijati Chuachua Rashid, ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuwaletea mradi wa maji ambao wanategemea utamaliza kabisa kero ya kutumia maji ya mito na kwenda kijiji jirani cha Nanyumbu kufuata maji.

Amehaidi kulinda mradi huo,ili uwe endelevu kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho na kueleza kuwa,siku za nyuma kuna baadhi ya wananchi waliowahi kuugua ugonjwa wa kipindu pindu kutokana na kutumia maji yasio safi na salama.

Mkazi wa kijiji cha Namijati Shuvaa Twaha alisema, manufaa ya mradi huo ni makubwa sana kwao na wanategemea utakuwa suluhisho la kumaliza migogoro ya ndoa inayotokea mara kwa mara katika jamii.

Aidha,amewaomba Wataalam wa Ruwasa kuwa karibu fundi anayejenga mradi huo ili aweze kukamilisha kazi kwa muda uliopangwa kwa sababu wamechoka kuendelea kutumia maji ya visima vya asili na kutembea umbali mrefu kufuata maji kwa ajili ya matumizi ya familia zao.

Kwa upande wake,Meneja wa Ruwasa wilaya ya Nanyumbu Simon Mchucha alisema,mradi huo unatekelezwa katika vijiji viwili vya Mitumbati na Namijati kwa gharama ya Sh.1,356,000,537.8.

Alisema,kati ya fedha hizo Sh.518,000,000 zimetolewa na serikali kuu kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid-19.na Sh. 838,000,537.8 ni fedha za mpango wa lipa kwa matokeo(P4R).

Alisema,mradi huo utahudumia wakazi 3,285 wa vijiji vya Mitumbati na Namijati na chanzo kikuu cha maji cha mradi ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita 15,800 kwa saa kilichopo kijiji cha Mitumbati.

Alisema,mradi wa Mitumbati-Chilunda unatekelezwa na mkandarasi kampuni ya Kharton Traders inayotekeleza kazi za ujenzi na ulazaji wa bomba kwa gharama ya Sh.643,320,022.8 ambapo ununuzi wa bomba,Jenereta na Pampu unafanywa na wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kwa gharama ya Sh.712,680,515

Mchucha alieleza kuwa,mradi umeanza kutekelezwa tarehe 29 Disemba 2021 na umepangwa kukamilika mwezi Mei 2022 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 60 ya utekelezaji wake.

Previous articleSPIKA WA BUNGE TULIA ACKSON AMPONGEZA RAIS SAMIA KUZINDUA FILAMU YA THE ROYAL TOUR
Next articleNABII DKT.JOSHUA ASISITIZA RAIS SAMIA NI KIONGOZI HODARI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here