Na: WAF- DOM
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa nchini Tanzania (Centre of Diseases Control – CDC) Dkt. Mahesh Swaminathan katika Ofisi za Wizara Jijini Dodoma.
Waziri Ummy Mwalimu ameishukuru CDC kwa kuendelea kuwa mshirika wa Karibu wa Serikali na Wizara ya Afya kwa kutoa ushirikiano na msaada katika mapambano dhidi ya Magonjwa mbalimbali ikiwemo Ugonjwa wa Virusi Vya Ukimwi, Kifua Kikuu, Malaria pamoja na UVIKO-19.
“CDC amekuwa mshirika wetu wa karibu katika mapambano dhidi ya magonjwa mbalimbali na katika kutekeleza afua za kuboresha ubora wa huduma za afya nchini Tanzania.” Amesema Mhe. Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy Mwalimu ametaka ushirikiano zaidi katika kuboresha na kuongeza huduma za maabara za afya ya jamii pamoja na kuboresha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa ili kuwezesha Serikali kuchukua hatua stahiki mapema zaidi na kuokoa maisha ya wananchi.
Waziri Ummy Mwalimu ameishukuru Serikali ya Marekani kupitia miradi na programu zinatokelezwa hapa nchini kwa kutoa msaada wa USD Milioni 22 kwa jili ya kusaidia Serikali katika mapambano dhidi ya UVIKO-19 na kuhamasisha wananchi kuchanja zaidi chanjo ya UVIKO-19.
Aidha Waziri Ummy Mwalimu ameiomba CDC kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kusaidia kupunguza uhaba wa rasilimali watu katika Kada za Afya kwa kutoa ajira za mikataba kwa Watanzania ili kuweza kupunguza pengo la ajira za Kada ya afya ambalo kwa sasa kuna uhaba wa asilimia 53.
Kwa upande wake Mkuregenzi Mkazi wa CDC nchini Dkt. Swaminathan ameishukuruku Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kuwapa mazingira rafiki na ushirikiano zaidi katika kupambana na kdhibiti magonjwa.
“Tunaamini tupo hapa sio kwajili ya kuzuia magonjwa kuingia marekani, ugonjwa ukitokea hapa Tanzania unaathari moja kwa moja kabla ya kwenda kwingine na ndio lengo letu kuu kushirikana kwa pamoja katika mapambano dhidi ya magonjwa mbalimbali.” Amesema Dkt. Swaminathan
Dkt. Swaminathan amesema kuwa CDC imekuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na Wizara ya Afya nchini katika mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa kutoa msaada wa dawa za kupunguza makali ya VVU, kushiriki katika tafiti mbalimbali zenye kulenga kupata tiba dhidi ya magonjwa mbalimbali pamoja na mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu, Malaria pamoja na ugonjwa wa UVIKO-19 nchini.
Dkt. Swaminathan amesema kuwa milango ya CDC iko wazi muda wote kwa kutoa ushauri wa kitaalam pamoja na rasilimali katika kusaidia Serikali kuweza kutoa huduma bora za tiba kwa wananchi.